IQNA

Utawala wa Kizayuni wafunga daraja la Bab al-Maghariba

14:37 - December 13, 2011
Habari ID: 2237818
Askari wa utawala haramu wa Israel jana Jumatatu walifunga daraja la Bab al-Maghariba linalounganisha Msikiti wa al-Aqsa katika eneo la kale la Quds Tukufu.
Kwa mujibu wa tovuti ya CPI, askari hao wamedai kuwa wamelazimika kufunga daraja hilo kutokana na amri iliyotolewa na meya wa Kizayuni wa mji wa Quds kwa hoja eti ya kulinda usalama wa raia.
Maafisa wa Palestina wamesema kuwa utawala huo ulikuwa na nia ya kuharibu daraja hilo tokea zamani lakini ulisita kutekeleza nia hiyo kutokana na malalamiko mengi ya Waislamu na taasisi za Kiislamu katika eneo hilo.
Wapalestina wanaonya kwamba hatua ya utawala haramu wa Israel ya kuharibu daraja hilo ni utangulizi wa kubomolewa Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas pia imetoa taarifa ikitaja hatua hiyo kuwa ni njama mpya ya Wazayuni dhidi ya Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa na kuwataka Waislamu wote duniani kufanya juhudi za kulinda matukufu ya Kiislamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Hamas imesema kwamba hatua hiyo ya Wazayuni ni katika mfululizo wa njama zinazofanywa kwa madhumuni ya kuwafukuza Wapalestina, ambao ni wakazi na wamiliki halisi wa Quds Tukufu na hatimaye kuufanya mji huo kuwa wa Mayahudi.
Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Jordan ni kundi jingine ambalo limelaani vikali hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa ni ukiukaji na dharau ya wazi dhidi ya matukufu ya Kiislamu huko Palestina. Imesisitiza kwamba utawala ghasibu wa Israel umekuwa ukizidisha harakati za kichochezi na kichokozi dhidi ya matukufu ya Kiislamu katika ardhi hizo kutokana na kimya cha jamii ya kimataifa. 914740
captcha