IQNA

Kikao cha 'Mapambano dhidi ya Ubaguzi wa Kidini' chafanyika Washington

16:06 - December 14, 2011
Habari ID: 2238487
Kikao cha Mapambano dhidi ya Ubaguzi wa Kidini ambacho kiliandaliwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na kuhudhuriwa na wawakilishi wa mashirika na taasisi za kimataifa kilianza siku ya Jumatatu mjini Washington, Marekani.
Kwa mujibu wa tovuti ya Ahram, kikao hicho cha siku mbili kilihudhuriwa na wawakilishi wa mashirika na jumuiya muhimu za kimataifa zikiwemo za OIC, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Washiriki wa kikao hicho kilichomalizika jana Jumanne walichunguza muswada nambari 16/18 ambao ulipasishwa mwaka jana na Baraza la Kimataifa la Haki za Binadamu mjini Genava Uswisi. Mswada huo unasisitiza juu ya kuendeshwa mapambano dhidi ya ubaguzi wa kidini, taasubi na utumiwaji mabavu kwa kutegemea thamani na itikadi za kidini.
Akizungumza katika kikao hicho, Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) amesema kuwa matokeo ya kikao hicho yatasaidia sana katika kuimarisha mazungumzo ya tamaduni tofauti na pia kuchangia juhudi za ulimwengu wa Kiislamu na Kimagharibi za kufikia msimamo mmoja kuhusiana na jinsi ya kupunguza chuki dhidi ya dini ya Kiislamu katika nchi za Magharibi.
Washiriki pia wamefanya juhudi za kuondoa vikwazo vinavyozuia utekelezwaji wa muswada uliotajwa ambao unasisitiza juu ya uhuru wa kujieleza. 914799
captcha