Kwa mujibu wa tovuti ya al-Alam, waandamanaji hao ambao walitoka katika mji wa Ras ar-Ruman walikusanyika mbele ya ubalozi huo kulalamikia siasa za serikali ya London za kuunga mkono vitendo vya jinai vinavyofanywa na ufalme wa Aal Khalifa dhidi ya raia wasio na hatia wa Bahrain.
Uungaji mkono wa serikali ya Uingereza kwa utawala wa Aal Khalifa katika kukandamiza maandamano ya amani ya Wabahraini ni jambo ambalo limeamsha hasira kubwa ya wananchi wa nchi hiyo dhidi ya serikali ya London. Askari wa Saudi Arabia na Imarati waliingia nchini Bahrain tarehe 14 Machi mwaka huu kwa lengo la kuusaidia utawala wa nchi hiyo kuzima kwa nguvu maandamano ya amani ya wananchi wanaopigania haki zao zinazokanyagwa waziwazi na utawala huo.
Kwa mujibu wa ripoti ya kamati ya uchunguzi iliyobuniwa kuchunguza ghasia hizo, askari wa Bahrain na wakigeni wanaoshirikiana na utawala wa nchi hiyo walitumia nguvu za ziada kukandamiza maandamano hayo. Kamati hiyo pia iliwatuhumu askari hao kwa kutesa na kuvunja haki za waandamanaji. Imetaka waandamanaji waliotiwa nguvuni na kuhukumiwa vifungo virefu kupunguziwa vifungo hivyo na pia waathirika wa siasa hizo za mabavu za utawala wa Bahrain kufidiwa kifedha. 916591