Taarifa hiyo inasema kuwa matukio hayo ya kusikitisha yanayotokea katika kipindi hiki nyeti katika historia ya Misri yanabainisha wazi kwamba kungali kuna baadhi ya watu nchini humo ambao hawaridhishwi na mapinduzi ya wananchi ambayo yanapigania uhuru, demokrasia na uadilifu wa kijamii nchini.
Taarifa hiyo imesisitiza kwamba matukio hayo ya kusikitisha yanathibitisha kwamba njama za watu hao waovu zitashindwa tu kwa kushikamana wananchi na thamani za Kiislamu na uhuru. Ikhwanul Muslimin imesema kwamba kutowekwa wazi matokeo ya uchunguzi wa matukio ya hivi karibuni na kutoadhibiwa wahusika wa matukio hayo, ni jambo linalowashajiisha wafitini na wachochezi wa vurugu kuendelea kutenda jinai dhidi ya taifa la Misri. Imesema matamshi ya kugongana yanayotolewa na watawala wa hivi sasa wa Misri yanachochea pia ghasia na machafuko nchini humo.
Taarifa ya Ikhwanul Muslimin imeendelea kusema kuwa kuna baadhi ya duru na vyombo vya habari vya kigeni vinavyochochea fitina, woga, mgongano na machafuko miongoni mwa Wamisri.
Awali Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon ilitoa taarifa ikilaani matukio ya fitina zinazochochewa na maadui wa Uislamu na mataifa ya Kiarabu na kuwataka wananchi wote wa Misri kuwa waangalifu na kutahadhari njama za maadui hao. 918210