Akibainisha suala hilo hapo jana Jumamosi, Khalid Nassiri, Waziri wa Habari na Msemaji wa Serikali ya Morocco amesema kwamba jarida hilo limefanya dharau hiyo kwa kisingizio cha kuchambua picha za kumvunjia heshima Mtume zilizochapishwa katika gazeti jingine la Ufaransa na kisha kusambaza nakala zake katika nchi za Kiarabu. Amesema kwa mujibu wa sheria za Kiislamu usambazaji wa picha zozote zinazohusiana na Mtume (saw) ni marufuku na kwa hivyo toleo la mara hii la jarida la Express halitauzwa nchini humo.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Waziri wa Habari wa Morocco amesema kwamba serikali imeyaonya magazeti yanayouzwa nchini humo kuzingatia kwa kina suala hilo kwa sababu wananchi wa Morocco wanafuatilia suala hilo kwa karibu sana.
Katika upande wa pili wachapishaji wa gazeti hilo wamekerwa na hatua hiyo ya serikali ya Morocco na kuilaani wakidai kwamba ni sensa isiyokubalika dhidi ya vyombo vya habari. 921896