IQNA

OIC yalaani machafuko Nigeria

16:05 - December 26, 2011
Habari ID: 2245668
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC Profesa Ekmeleddin Ihsanoglu amelaani hujuma zilizofanywa hivi karibuni na kundi la Boko Haram kaskazini mwa nchi hiyo katika maeneo ya Damaturu, Patiskum na Maiduguri.
Makumi ya watu waliuawa katika hujuma hizo.
Katibu Mkuu wa OIC pia ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga na vile vile kwa watu na serikali ya Nigeria.
Ehsanoglu amekosoa machafuko yanayofanywa na wanamgambo wa Boko Haram katika maeneo kadhaa ya Nigeria. Ametoa wito kwa wanamgambo hao kufanya mazungumzo na serikali ili kukomesha umwagaji damu na masaibu ya wananchi. Aidha amewataka Wanigeria wote kushirikiana na serikali katika kurejesha utulivu nchini humo.
Kutokana na kufanana fikra zao na kundi la Taliban la Afghanistan na mtandao wa al Qaida, kundi hilo la Boko Haram limepewa jina la Taliban wa Nigeria. Miongoni mwa masuala yanayopingwa na kundi hilo ni mfumo wa Kimagharibi wa masomo. Hata neno Boko Haram nalo ambalo linatokana na lugha ya Kihausa lina maana hiyo hiyo. Neno "Boko" maana yake ni mfumo wa kipagani wa Magharibi na mfumo wowote usio wa Kiislamu wa masomo, na neno "Haram" nalo lina maana ya kitu cha haramu. Hivyo tunaweza kusema kuwa, "Boko Haram" lina maana ya "mfumo wa kipagani wa masomo ni haramu."
922872
captcha