Taarifa iliyotolewa na Hamas imeonya kuhusu rasimu ya sheria ya kibaguzi ya Israel ya kuutangaza mji wa Quds kuwa mji mkuu pekee wa Israel.
Hamas imeongeza kuwa, 'utawala wa Kizayuni utabeba lawamu kuhusu natija ya sheria hiyo ya kutangaza Quds Tukufu kuwa mji mkuu wa Israel'. Hamas imeongeza kuwa rasimu hiyo ya sheria imewasilishwa katika hali ambayo utawala haramu wa Israel unaendeleza hujuma zake za kinyama dhidi ya ardhi za Palestina na kuyavunjia heshima matukufu ya kidini ya Wapalestina.
Hamas imesisitiza kuwa Quds ni mstari mwekundu wa Wapalestina na kuongeza kuwa , 'Quds ni ya Wapalestina, taifa la Palestina na wakazi wa Quds wataendelea kulinda haki zao na maamuzi ya utawala wa Kizayuni hayatabadilisha historia na ukweli wa mambo.
Naye Mufti wa Quds huko Palestina amesema kuwa, mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuutangaza mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala huo ghasibu ni batili na inayokinzana na sheria.
Sheikh Muhammad Hussein amesema, hata kama mpango huo utapasishwa na Bunge la utawala haramu wa Israel bado utakuwa batili na usiokubalika kwani umetoka kwa utawala vamizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Wakati huo huo, Ismail Hania Waziri Mkuu wa serikali halali ya Palestina iliyochaguliwa na wananchi amesema kwamba, uamuzi huo wa Israel ni batili na kusisisitiza kwamba, Quds ni mji mkuu wa Palestina na daima ni kipenzi cha nyoyo za mamilioni ya Waislamu katika nchi za Kiislamu.
922997