Huku akisisitiza kwamba wananchi wa Palestina kamwe hawatafumbia macho hata shibiri moja ya ardhi yao, Ismail Haniya, Waziri Mkuu wa serikali halali ya Palestina ametaka kubuniwa kwa jeshi la Kiarabu kwa jina la Jeshi la Quds.
Haniya ambaye yuko safarini nchini Sudan aliyasema hayo jana Jumamosi aliposhiriki katika kikao cha kimataifa cha Quds mjini Khartoum akiwa na Nafi' Ali Nafi' Makamu wa Rais wa Sudan na shakhsia wengine wa kimataifa.
Huku akisisitiza kwamba Quds Tukufu ni ya Wapalestina na kwamba wanatambua ukombozi wake kutoka mikononi mwa maghasibu wa Kizayuni kuwa jukumu lao kubwa, Haniya amesema kuwa wananchi wa Palestina hawatafumbia macho hata nchi moja ya ardhi yao wala kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel.
Amesema wakati umewadia wa kila nchi kuunda jeshi maalumu la kukomboa Quds. Amesema mwamko wa Kiislamu unaoonekana sasa ulimwenguni ni tukio muhimu katika historia ya umma wa Kiislamu.
Waziri Mkuu wa Palestina amesema licha ya utawala haramu wa Israel kufanya hujuma za mara kwa mara dhidi ya mji huo na kuimarisha njama za kuuyahudisha lakini Wapalestina wamesimama imara katika kulinda thamani na utukufu wake.
Haniya ameishukuru serikali ya Sudan kutokana na uungaji mkono wake kwa suala zima la Palestina. 926509