IQNA

Usalama waimarishwa Karbala kabla ya Arbaini ya Imam Hussein (as)

15:50 - January 04, 2012
Habari ID: 2251064
Baraza la Mkoa wa Karbala limetangaza kuwa hatua za usalama zimeimarishwa katika mkoa huo katika kukaribia wakati wa maombolezo ya Arbaini ya Imam Hussein (as).
Kwa mujibu wa televisheni ya al-Faihaa, hayo yamesemwa na Muhammad al-Musawi, mkuu wa Baraza la Mkoa wa Karbala na kuongeza kuwa askari usalama na ofisi za huduma kwa wafanyaziara zimewekwa tayari kwa ajili ya kuwapokea waombolezaji wa makumbusho ya kuuawa shahidi Imam Hussein (as).
Muhammad al-Musawi ameongeza kuwa viongozi wa mkoa huo wamefanya vikao tofauti kwa ajili ya kutoa mafunzo na miongozo ya dharura kwa maafisa usalama na wahudumu kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wafanyaziara na waombolezaji wa Arbaini ya Imam Hussein (as).
Amesema, idara maalumu imeanzishwa kwa madhumuni ya kudhamini usalama wa waombolezaji na kudhibiti harakati zao.
Maafisa usalama katika mji huo wamesema kuwa watatekeleza hatua za usalama kama zile zilizotekelezwa wakati wa maombolezo ya tarehe 10 Muharram ambapo kasoro zitaondolewa na baadhi ya marekebisho ya dharura na ya kistratejia yatafanyika.
Maafisa hao wameongeza kuwa hadi sasa vyombo vya usalama vya Iraq vimegundua na kusambaratisha mitandao kadhaa ya kigaidi pamoja na kuwatia mbaroni wahusika wa mitandao hiyo. 928332
captcha