IQNA

Dhulma ya Utawala wa Saudia dhidi ya Mashia

14:54 - January 08, 2012
Habari ID: 2252983
Ayatullah Nimr Baqir Aal Nimr, hatibu wa Swala ya Ijumaa ya mkoa wenye Mashia wengi wa al-Awamiya nchini Saudi Arabia ametaja amri ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hiyo ya kutiwa nguvuni raia wa Kishia 23 kuwa ni ya kidhulma na kitaasubi.
Akizungumza hivi karibuni katika Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Imam Hussein (as) katika mji wa al-Awamiya, Ayatullah Nimr amesema kuwa siku itafika ambapo watu wote watawajibika kujibu maswali mbele ya Mwenyezi Mungu Muadilifu kuhusiana na matendo yao.
Amesema madhalimu humu duniani hawatakuwa na uwezo wa kusimama mbele ya Jamii ya Kiislamu wala mahakama ya uadilifu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama. Amesema utawala wa Saudi Arabia umewaua vijana wa Kishia na kisha kuwatia wengine nguvuni kwa kuwasingizia kuwa ndio waliohusika na mauaji hayo.
Amesema licha ya kuwa watawala wa Saudia wanatambua vyema kwamba wao ni madhalimu lakini hawakubali wala kustahamili kumsikia mtu yoyote akitamka ukweli huo kuwahusu. Amemaliza kwa kusema kuwa madhalimu na watu wanaoshirikiana nao hawana nafasi yoyote miongoni mwa wananchi na kwamba jamii haiwakubali kabisa. 930599
captcha