IQNA

Kongamano la “Vijana na Mwamko wa Kiislamu” Tehran

14:48 - January 30, 2012
Habari ID: 2264827
Kikao cha kwanza cha kimataifa cha "Vijana na Mwamko wa Kiislamu" kilianza jana Jumapili hapa mjini Tehran kikiwashirikisha zaidi ya vijana wasomi 1,600 kutoka ndani na nje ya Iran. M
Miongoni mwa mada kuu za kikao hicho ni mustakbali wa mwamko wa Kiislamu, Mapinduzi ya Kiislamu, vigezo na matunda yaliyopatikana pamoja na vijana na wimbi la mwamko wa Kiislamu. Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika hotuba ya ufunguzi wa kikao hicho kuwa, uhuru, uadilifu na heshima ni haki ya mataifa yote duniani. Amesema, dunia hivi sasa inakabiliwa na hali mbaya sana huku nyufa katika vipato vya watu zikizidi kuwa kubwa. Amesema dunia hivi sasa inakabiliwa na mashindano ya kujilimbikizia silaha hatari, uwezekano wa watu wabaya kuidhibiti dunia, kuzidi vitendo vya kibeberu vya baadhi ya madola duniani, sambamba na kuzidi kukosekana uadilifu, uhuru na mshikamano kati ya wanaadamu.
Rais Ahmadinejad amesema, kama tumeona nchi nyingi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika zilikuwa zinatawaliwa na madikteta na hadi hivi sasa baadhi yake zinaendelea kutawaliwa na tawala za kiimla tujue kuwa chanzo chake ni uingiliaji wa madola ya kibeberu na utawala wa Kizayuni katika masuala ya ndani ya nchi za maeneo hayo.
Naye Dk. Ali Akbar Velayati, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu ambaye pia ni Mshauri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa amesema katika hotuba yake kuwa mwamko wa Kiislamu si vyema kuuona kuwa ni jambo lililozuka hivi karibuni. Amesema, mapambano dhidi ya madola ya kibeberu na kupinga uingiliaji wa kigeni katika mambo ya ndani ya mataifa ya Kiislamu, kupigania haki za taifa la Palestina pamoja na kuhuisha na kutia nguvu utambulisho wa Kiislamu ni katika mambo yaliyokuwa yanatakiwa muda mrefu na mataifa ya Kiislamu katika nchi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.
Dakta Velayati amesema miongoni mwa sifa za kipekee za matukio ya eneo hilo ni kuwa kwake na sura ya Kiislamu, kuwa kwake harakati za wananchi, kupinga kwake dhulma na ubeberu, kufanyika kwake kwa amani na kupigania kwake uhuru na kujikomboa kutoka katika makucha ya watawala vibaraka.
Naye Ammar Hakim, Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq amesema katika hotuba yake kuwa mabeberu wanafanya njama za kujaribu kuzirejesha madarakani tawala za vibaraka madikteta na ameyatahadharisha mataifa ambayo yamefanikiwa kuwapindua watawala vibaraka, yawe macho kuhusu njama hizo za mabeberu. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kushikamana na Uislamu, kuhakikisha malengo ya wananchi wanamapinduzi yanafikiwa, kufanya kazi bila kuchoka katika juhudi za kuleta maendeleo na kudumisha mshikamano ni miongoni mwa mambo muhimu sana yanayopaswa kuzingatiwa na mataifa ambayo tayari yamefanikiwa kuwapinduwa watawala madikteta.
Weledi hao wa mambo aidha wanasema, istikama na kutotetereka katika harakati zao ni jambo muhimu pia kwa yale mataifa ambayo bado hayajafanikiwa kuwang'oa madarakani vibaraka wa madola ya kibeberu. Alaakullihaal, kufanyika vikao kama hivi ni miongoni mwa masuala muhimu ya kuweza kuzikurubisha pamoja fikra za vijana wanamapinduzi kwa ajili ya kujenga mustakbali bora wa ulimwengu wa Kiislamu.
942621

captcha