IQNA

Sherehe za Miladun Nabii SAW kufanyika Uganda

14:21 - February 04, 2012
Habari ID: 2267719
Kwa mnasaba wa maadhimisho ya Miladun Nabii SAW, Mtume Mtukufu wa Uislamu na Imam Ja'far Sadiq AS, sherehe maalumu zimeandaliwa Februari 10 katika mji wa Jinja nchini Uganda.
Akizungumza na IQNA, Sheikh Suleiman ambaye alihitimu katika Chuo Kikuu cha Al Mustafa SAW na ambaye ni Imamu katika Msikiti wa Mashia Jinja amesema sherehe adhimu zimepangwa kwa mnasaba wa Miladun Nabii mwaka huu.
Amesema sherehe hizo zitaanza baada ya sala za dhuhrein na kuendelea hadi maghribein. Mji wa Jinja ndio wa pili kwa ukubwa nchini Uganda.
Ameongeza kuwa tarehe 17 Rabiul Awwal kote Uganda, Waislamu Mashia na Masuni watafanya sherehe mbalimbali za Maulidi ya Mtume na mjukuu wake Imam Ja'far Sadiq AS ambazo zitajumuisha qiraa ya Qur'ani Tukufu, hotuba kuhusu sira ya Mtume SAW na Qasida. Waislamu nchini Uganda pia wataadhimisha wiki ya Umoja wa Kiislamu ambayo huanza tarehe 12-17 Rabiul Awwal.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.
Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shia linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikitangaza kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

946053
captcha