IQNA

Umoja hitajio muhimu la Umma wa Kiislamu

11:53 - February 06, 2012
Habari ID: 2269435
Sheikh Mahmoud Ashur, Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Ukurubishaji wa Madhehebu ya Kiislamu na mwanazuoni mashuhuri wa chuo cha kidini cha al-Azhar amesema kuwa hii leo Umma wa Kiislamu unahitaji kuwa na umoja na mshikamano kuliko wakati mwingine wowote.
Amewataka viongozi wa Kiislamu kuwa macho mbele ya njama za maadui na kuimarisha umoja wa Waislamu.
Akizungumza hivi karibuni kupitia televisheni ya al-Alam ya nchini Iran, Sheikh Ashur amewatahadharisha Waislamu dhidi ya njama zinazofanywa hivi sasa na maadui wa Uislamu kwa lengo la kuzusha fitina na mifarakano miongoni mwa Waislamu. Amesisitiza kuwa maadui daima wamekuwa wakifanya njama za kuwagonganisha Waislamu kupitia mifarakano hiyo.
Amesema, Uislamu daima unawasihi wafuasi wake kuwa na umoja na kuimarisha upendo kati yao. Amewataka Waislamu kutekeleza vyema majukumu yao ya kidini na kuwa macho mbele ya njma za maadui. Ameongeza kwamba Waislamu wanapasa kuwapuuza watu wanaowakufurisha Waislamu wenzao kwa sababu hawajui lolote katika mafundisho ya Kiislamu yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wake (saw).
Sheikh Ashur amesema kama alivyosema Mtume Mtukufu (saw) kwamba Umma wa Kiislamu ni mfano wa viungo tofauti vya mwili mmoja ambapo kiungo kimoja kinapopata maumivu basi viungo vingine vya mwili huo huathirika na kukosa utulivu. 947693
captcha