IQNA

OIC yasisitiza umoja kwa kutegemea mafundisho ya Qur'ani

15:24 - February 06, 2012
Habari ID: 2269437
Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OI)C ametoa taarifa ya kuwapongeza Waislamu wote duniani kwa mnasaba wa kuwadia maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Mtume Mtukufu (saw) na kuwataka walinde umoja wao kwa msingi wa mafundisho ya Qur'ani Tukufu.
Amesema tukio la kuzaliwa Mtume ulikuwa mwanzo wa zama mpya katika historia ya mwanadamu na ujumbe wa rehema na amani kwa walimwengu. Ameendelea kusema kuwa Mtume Muhammad (saw) alikuwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu ambaye aliwaonyesha wanadamu njia sahihi na nyoofu ya saada.
Ihsanoglu amewataka Waislamu ambao katika siku hizi tukufu wanasherehekea siku ya kuzaliwa Bwana Mtume (saw) wazingatie sira, maisha na mafundisho yake yenye thamani kubwa pamoja na kudumisha njia yake ya wokovu wa mwanadamu.
Katika sehemu nyingine ya ujumbe huo, Ihsanoghl amesema kwamba Umma wa Kiislamu hii leo unapitia kipindi kigumu na nyeti na kwamba sherehe za maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Mtume (saw) inapasa kuwa fursa nzuri ya kuwawezesha Waislamu kubadilishana mawazo kuhusu njia za kutatua matatizo na changamoto nyingi zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu.
Amewataka Waislamu wote ulimwenguni kudumisha udugu wa Kiislamu na kujiepusha na mivutano na ugomvi baina yao kwa kutegemea mafundisho ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Amesisitiza udharura wa kulindwa utambulisho wa Kiislamu wa Palestina na hasa Msikiti wa al-Aqsa na Quds Tukufu, kibla cha kwanza cha Waislamu ambacho amekitaja kuwa zawadi maalumu ya Mwenyezi Mungu kwa Waislamu.
Katibu Mkuu wa OIC ameelezea matumaini yake kwamba Umma wa Kiislamu utaungana kwa madhumuni ya kuikomboa Palestina. 948197
captcha