IQNA

China kujenga jumba la kuhifadhi Qur'ani ya kale

16:23 - February 18, 2012
Habari ID: 2276018
Viongozi wa eneo la Dongjiang kaskazini magharibi mwa China wameamua kujenga jumba la kuhifadhi nakala ya Qur'ani ya kale ili kulinda turathi hiyo ya thamani ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa tovuti ya ZeeNews, karibu yuan milioni nne za China zitatumika katika ujenzi wa jumba hilo ambao utachukua chini ya mwaka mmoja kukamilika. Ujenzi huo unatazamiwa kuanza katika kipindi cha miezi miwili ijayo.
Nakala ya Qur'ani hiyo iliyogunduliwa mwaka 2009 katika eneo la Dongjiang ina kurasa 536 na kwa mujibu wa maoni ya wataalamu wa China, Uingereza na Japan ambao wameichunguza, nakala hiyo iliandikwa kati ya karne ya 9 na 11 Miladia.
Jumba hilo la kuhifadhia mambo ya kale lina lengo la kutumia mbini za kisasa kabisa katika kuhifadhi Qur'ani hiyo ya kale pamoja na maandishi mengine ya mkono.
Akizungumzia suala hilo Makingfang mmoja wa viongozi wa Kiislamu wa eneo hilo amesema kuwa nuskha hiyo itahifadhiwa katika jengo litakalojengwa, kama turathi ya kiutamaduni na kitaifa. Amesema kumekuwepo na mapendekezo mengi ya kununuliwa kitabu hicho cha mbinguni lakini viongozi wa Kiislamu wamekataa kukiuza kwa hoja kuwa thamani yake ni kubwa mno kwa kadiri kwamba haiwezi kuainishiwa bei.
Wanasema kuwa kitabu hicho kitakuwa na nafasi muhimu katika uchunguzi wa historia ya Kiislamu nchini China, historia ya makundi ya kikabila ya Dongjiang pamoja na utamaduni wa China. 955121
captcha