IQNA

Wahifadhi kutoka nchi 29 washiriki fainali ya Mashindano ya Kuhifadhi Qur’ani Tukufu Afrika Kusini

17:11 - September 19, 2025
Habari ID: 3481250
IQNA – Hatua ya mwisho ya mashindano ya kimataifa ya kuhifadhi Qur’ani Tukufu imeanza Alhamisi katika mji mkuu wa Afrika Kusini, ikiwakutanisha washiriki kutoka nchi 29.

Mashindano haya yanayojulikana kama Mashindano ya Mfalme Salman bin Abdulaziz ya Kuhifadhi Qur’ani Tukufu na Sunnah ya Mtume (SAW) barani Afrika, yameandaliwa mjini Pretoria na Wizara ya Mambo ya Kiislamu ya Saudi Arabia kupitia kitengo cha kidini cha ubalozi wao nchini Afrika Kusini.

Kwa mwaka huu, jumla ya washiriki 44 kutoka nchi 29 za Afrika wanashiriki, ambapo 29 wanashindana katika kipengele cha kuhifadhi Qur’ani Tukufu na 15 katika kipengele cha Sunnah ya Mtume (SAW).

Washiriki hawa wamefuzu hadi fainali baada ya kupita hatua za awali zilizowahusisha zaidi ya washiriki 80,000 kutoka taasisi na shule 1,840 za kuhifadhi Qur’ani.

Mashindano haya yamegawanywa katika vipengele vya kuhifadhi Qur’ani yote, kuhifadhi sura kumi, kuhifadhi sura tano, pamoja na kipengele maalum cha Sunnah ya Mtume (SAW), ambapo zawadi tatu zimetengwa kwa kila kipengele.

Hatua ya mwisho inahukumiwa na jopo la majaji waliobobea katika elimu ya Qur’ani na Uislamu kutoka Saudi Arabia na Afrika Kusini.

Lengo kuu la mashindano haya ni kuwahamasisha vijana kuhifadhi, kuelewa na kutafakari Qur’ani Tukufu, kuimarisha roho ya mashindano ya heshima miongoni mwa wahifadhi, kukuza uhusiano wa dhati na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah ya Mtume Muhammad (SAW), kuendeleza msimamo wa wastani, na kusambaza mafundisho ya Uislamu kwa hekima na busara.

4305750
captcha