Mwenyekiti wa zamani wa chama cha an Nadha cha Tunisia amelitaka bunge la kwanza huru la nchi hiyo kubuni katiba ya Kiislamu na kusema katiba mpya ya Tunisia inapaswa kubuniwa kwa kutegemea Qur'ani Tukufu, Suna za Mtume na Sheria za Kiislamu.
Sadiq Shourou ambaye alikuwa akihutubia kikao cha Kamati ya Kubuni Misingi na Kurekebisha Katiba ya Tunisia amesema kamati hiyo inawajibika kubuni katiba mpya kwa kutilia maanani vigezo vikuu vitatu.
Ameongeza kuwa katiba hiyo inapaswa kubuniwa kwa kutegemea Qur'ani, Suna na ijmaa au muafaka wa maulamaa wa umma wa Kiislamu.
Shourou amesema kuwa misingi hiyo mitatu inakubaliwa na maulamaa wote wa Kiislamu na kwa kuwa fikra za wanadamu zinabadilika na si thabiti, kuna udharura wa kutegemea sheria za Mwenyezi Mungu katika kubuni katiba mpya ya Tunisia.
Hotuba ya Sadiq Shourou imepingwa na vyama vingi vyenye misimamo ya kiliberali vinavyodai kuwa mambo hayo yanapinga na uundwaji wa serikali inayonasibiana na zama hizi. 956014