IQNA

ISESCO yalaani uchimbaji katika Msikiti wa al-Aqsa

15:53 - February 21, 2012
Habari ID: 2277995
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni wa Kiislamu (ISESCO) jana Jumatatu lilitoa taarifa likilaani siasa za utawala haramu wa Israel za kuharibu msikiti mtukufu wa al-Aqsa kwa kuendelea kuchimba mashimo na mitaro pembeni ya msikiti huo mtakatifu.
Kwa mujibu wa tovuti ya ISESCO kuendelea uchimbaji huo kwa kisingizio cha kujengwa hekalu bandia la Nabii Suleiman (as) ni hatari kubwa kwa turathi hiyo muhimu ya Kiislamu.
Shirika hilo limeunga mkono ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Wakfu na Turathi za Kiutamaduni ya Msikiti wa al-Aqsa. Taarifa ya ISESCO inasema kwa kuendelea kuchimba njia ya chini kwa chini iliyo na urefu wa mita 3000 chini ya eneo hilo la ibada, utawala haramu wa Israel una lengo la kuharibu kibla hicho cha kwanza cha Waislamu na kujenga sehemu yake vituo vya kibiashara na hekalu la Mayahudi.
Imesema utawala huo umekuwa ukifanya juhudi za kuyahudisha Quds Tukufu kwa kuharibu daraja la Bab al-Maghariba na kujenga hapo daraja la kijeshi. Isesco imelitaka Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kuchukua hatua za haraka kwa lengo la kusimamisha mara moja uharibifu unaofanywa na utawala wa Israel dhidi ya matukufu ya Kiislamu katika ardhi unazozikalia kwa mabavu za Palestina.
Limelitaka shirika hilo la Umoja wa Mataifa kutoruhusu utawala huo kutumia vibaya kimya cha jamii ya kimataifa katika kudumisha jinai zake katika ardhi hizo na hasa kuhusiana na suala la kuteketeza na kuharibu misikiti na makaburi ya Kiislamu. 957377
captcha