IQNA

OIC yalaani hujuma dhidi ya matukufu ya Wakristo huko Quds

12:19 - February 23, 2012
Habari ID: 2279344
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Uhirikiano wa Kiislamu amelaani vikali shambulio lililofanywa na Wazayuni wenye misimamo mikali dhidi ya Kanisa la Baptist huko katika mji mtakatifu wa Quds.
Kwa mujibu wa tovuti ya OIC, Ekmeleddin Ihsanoglu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo amelaani vikali hujuma ya Mayahudi wenye misimamo ya kupindukia mipaka dhidi ya kanisa hilo pamoja na maandishi yao ya matusi dhidi ya Nabii Isa na mama yake Maryam (as) kwenye kuta za kanisa hilo.
Huku akiashiria kuendelea kwa vitendo hivyo vya dharau na matusi vya Mayahudi dhidi ya matukufu ya Kiislamu na Kikristo katika mji huo Ihsanoglu amesema kuwa utawala haramu wa Israel ndio unaopaswa kubebeshwa jukumu la vitendo hivyo vya kuchukiza na vya kibaguzi. Ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kwa madhumuni ya kutetea maeneo matakatifu ya Wapalestina na kuulazimisha utawala huo usimamishe ukandamizaji dhidi ya watu wasio na hatia na wakati huohuo kutii sheria za kimataifa mara moja.
Katika upande wa pili Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, pia imetoa taarifa ikilaani vikali hujuma ya Mayahudi walio na misimamo ya kupindukia mipaka dhidi ya matukufu ya Waislamu na Wakristo. Hamas imesema kuwa huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na misingi ya dini za mbinguni jambo linalothibitisha wazi ubaguzi wa utawala huo haramu. 958560
captcha