Dkt. Mohammad Baqer Khorramshad ameyasema hayo mjini Dar es Salaam alipokutana na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania Profesa Makame Mbarawa. Amesema ustawi wa kasi wa Iran katika uga wa sayansi na teknolojia ni matokeo ya juhudi na ubunifu wa wasomi na wanasayansi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Aidha amesisitiza juu ya azma ya ICRO ya kuimarisha uhusiano na Tanzania na kuongeza kuwa shirika hilo litatoa msaada wa masomo kwa wanafunzi 7 wa Tanzania bara na watatu wa Zanzibar.
Khorramshad aidha ameashiria uwezo wa Iran katika sekta kama vile utamaduni wa Kiislamu, ustaarabu, nano teknolojia, mawasiliano ya satalaiti na kilimo na kusema Iran iko tayari kubadilishana uzoefu wake huo na Tanzania.
Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Tanzania Profesa Makame Mbarawa amesisitiza azma ya nchi yake ya kuimarisha uhusiano wa kiutamaduni na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema Kwa kuzingatia mahitajio mengi ya Tanzania katika sekta mbalimbali, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaweza kuwa chanzo kizuri cha kupata uwezo wa kisayansi.
959512