IQNA

OIC yalaani mashambulio ya utawala wa Kizayuni Ghaza

13:35 - March 12, 2012
Habari ID: 2290123
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imetoa taarifa ya kulaani vikali mashambulio ya jinai yaliyofanywa hivi karibuni na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa tovuti ya jumuiya hiyo, Ekmeleddin Ihsanoglu Katibu Mkuu wa OIC amelaani vikali mashambulio hayo na kusema kwamba jinai hiyo ambayo hadi sasa imepelekea kuuawa shahidi Wapalestina 12 na kujeruhiwa wengine zaidi ya 21 ni jinai ya kivita na kinyama inayokiuka wazi misingi na sheria za kimataifa. Amesema kuendelea kwa mashambulio kama hayo ambayo yanatekelezwa na askari chokozi wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia kutazidisha mivutano na ghasia katika Mashariki ya Kati, jambo ambalo amesema linaenda kinyume na haki za binadamu na sheria za kimataifa.
Katibu Mkuu wa OIC ameendelea kusema kuwa utawala haramu wa Israel ndio unapasa kubebeshwa lawama za jinai zote zinazotekelezwa dhidi ya Wapalestina na kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Kamati ya Pande Nne ya Amani ya Mashariki ya Kati zinapasa kutekeleza vyema majukumu yao kuhusiana na wananchi madhlumu wa Palestina.
Katibu Mkuu wa OIC amesisitiza kwamba taasisi mbili hizo zinapasa kuchukua hatua za dharura kwa madhumuni ya kusimamisha mara moja hujuma za mara kwa mara za utawala haramu wa Tel Aviv dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. 970209
captcha