Kwa mujibu wa televisheni ya nchi hiyo ya al-Manar, wanazuoni hao wamesema katika taarifa hiyo kwamba utawala haramu wa Israel umekuwa ukikiuka wazi haki za binadamu kwa kadiri kwamba kunyamazia kimya jinai hizo ni hiana ya wazi kwa umma wa Kiislamu.
Jumuiya hiyo imeongeza kwamba jinai za Israel dhidi ya watu wa Gaza zinatekelezwa katika hali ambayo Ehud Barak, Waziri wa Vita wa utawala huo haramu ametangaza wazi kuridhishwa na mauaji hayo ya kinyama ambayo amesema yanathibitisha kwamba silaha za mauaji ya utawala huo zinafanya kazi vizuri.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba inasikitisha kuona kuwa mashambulizi hayo ya kinyama yanafanyika katika hali ambayo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imekuwa ikifanya vikao visivyo na faida yoyote kwa watu wa Palestina na badala yake kudhoofisha harakati za mapambano ya Kiislamu dhidi ya utawala huo kwa kusisitiza kutumwa askari wa kimataifa nchini Syria.
Imesema inasikitisha kuona kuwa jumuiya hiyo haichukui msimamo kama huo wa kutaka kutumwa askari wa nchi za Kiarbu huko Israel kwa lengo la kuwasaidia Wapalestina dhidi ya jinai za kinyama zinazofanywa dhidi yao mara kwa mara na utawala haramu wa Israel. Imesema watawala vibaraka wa nchi za Kiarabu wamekuwa wakisisitiza kutumwa askari wa kigeni nchini Syria ili kuidhoofisha serikali ya nchi hiyo ambayo inaunga mkono mapambano ya Kiislamu dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.
Mashambulio mapya ya anga ya utawala huo ambayo yalianza siku ya Ijumaa tarehe 9 Machi dhidi ya Ukanda wa Gaza yamepelekea kuuawa kwa watu kadhaa na kujeruhiwa wengine wengi. 971012