IQNA

Waafghani wapongezwa kwa kuitetea Qur'ani

16:13 - March 17, 2012
Habari ID: 2292721
Hatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amelaani kitendo cha kishenzi kilichofanywa na vikosi vya jeshi la Marekani cha kuchoma moto nakala kadhaa za Qur'ani Tukufu na kuwaua bila ya hatia raia wa Afghanistan. Ayatullah Muhammad Imami Kashani amesema muda wa kuondoka vikosi vamizi nchini Afghanistan umewadia.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya hapa mjini Tehran Ayatullah Muhammad Imami Kashan amesifu kusimama kidete Waislamu wa Afghanistan na kuonyesha hasira zao kali, kufuatia kitendo hicho. Ameongeza kuwa wanajeshi wa Marekani wamewaua kiholela raia wa Afghanistan ili kujaribu kuwasahaulisha walimwengu kitendo chao kiovu cha hapo awali cha kuteketeza moto nakala za Qur'ani Tukufu.
Amesema kuwa, baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati zinazofuata kibubusa siasa za nchi za Magharibi, zimeazimia kuuzima kwa kila hali mwamko wa Kiislamu.
Akiashiria mapinduzi ya wananchi nchini Bahrain na njama za Saudi Arabia za kuendelea kufanya mauaji dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo, Ayatullah Kashani amesema, Saudia ambayo inaungwa mkono na Marekani inafanya kila njama za kuyazima mapinduzi ya wananchi nchini Bahrain kwa kuwaita wananchi wa nchi hiyo kuwa eti wanapingana na Uislamu na Uarabu.
Akijibu tuhuma hizo za viongozi wa Saudia dhidi ya wananchi wa Bahrain, Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amesema, harakati za wananchi wa Bahrain hazitofautiani hata kidogo na harakati za wananchi kama zile za Tunisia na Misri.
972916
captcha