Kwa mujibu wa tovuti ya 'levif', baraza hilo limeongeza kuwa: "Tunalaani vikali kitendo hicho cha uhalifu na kutangaza kuwa kitendo hicho kinakiuka mafundisho ya Uislamu na maamrisho ya madhehebu yote'.
Taarifa hiyo imeendelea kusema: 'Tunatoa wito kwa Waislamu wote waishio Ubelgiji kudumisha umoja na mshikamano wao na wasitumbukie katika fitina. Raia Waislamu wanapaswa kudumisha heshima ya pande zote na kutowaruhusu maadui wa Uislamu kufikia malengo yao'.
Itakumbukwa kuwa Jumatatu wiki iliyopita Imamu wa Msikiti wa Imam Ridha AS Ubelgiji ameuliwa kikatili na watu wanaosadikiwa kuwa na itikadi za Kiwahabi katika mji mkuu wa nchi hiyo Brussels.
Kwa mujibu wa tovuti ya tf1, Bi. Isabelle Praile Naibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Ubelgiji alisema, 'siku ya Jumatatu tarehe 12 Machi Msikiti wa Imam Ridha AS uliteketezwa kwa moto na watu wenye misimamo mikali ya Kiwahabi'.
Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo la kusikitisha amesema: 'Karibu saa moja usiku Jumatatu, watu waliushambulia Msikiti wa Imam Ridha AS na kutupa bomu aina ya 'molotov cocktail' (bomu la petrol) ndani ya msikiti na ukaanza kuteketea kisha wakafunga milango yote na baada ya hapo Imamu wa Sala ya jamaa pamoja na muumini mwingine walikufa shahidi kutokana na moshi'.
Polisi nchini Ubelgiji wamesema wamemkamata mtu mwenye asili ya Morocco aliye na umri wa miaka 47 kuhusiana na hujuma dhidi ya msikiti huo. Imedokezwa kuwa jina lake ni Dadou. Mtu huyo ambaye amekiri kufuata madhehebu ya Kiwahabi amedai kuwa ameuteketeza msikiti huo kutokana na kuwa wanaoswali hapo wanaiunga mkono serikali ya Syria.
973145