IQNA

Amnesty International: Waislamu wanabaguliwa Ulaya

22:58 - April 24, 2012
Habari ID: 2312028
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limelaani vikali ubaguzi unaofanywa dhidi ya Waislamu barani Ulaya na jinsi chuki dhidi ya Uislamu zinavyotumiwa kwa ajili ya maslahi ya kisiasa.
Ripoti ya Amnesty International imejikita zaidi kuhusu hali ya Waislamu katika nchi za Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi, Uhispania na Uswisi na kuzitaka nchi za Ulaya kukabiliana na ubaguzi dhidi ya Waislamu hususan katika taasisi za elimu na maeneo ya kazi.
Mtaalamu wa Amnesty Marco Perolini amesema vyama vya siasa barani Ulaya vimekuwa vikichochea propaganda chafu dhidi ya Uislamu kwa ajili ya kupata kura za wananchi. Ameongeza kuwa wanawake wa Kiislamu wananyimwa kazi na wasichana Waislamu wanazuiwa kuingia mashuleni kwa sababu tu ya kuvaa mavazi ya kitamaduni kama mitandio. Perolini amesisitiza kuwa Waislamu wanaume hunyimwa kazi kwa sababu tu ya kuwa na ndevu. Amesisitiza kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira katika nchi za Ulaya ni kikubwa mno katika jamii za Waislamu.
Amnesty pia imekosoa hatua ya kubanwa uhuru wa Waislamu katika nchi za Ulaya hasa utekelezaji wa sala na kusema kuwa nchini Uswisi kumepasishwa sheria inayopiga marufuku ujenzi wa minara ya misikiti na huko Uhispania katika jimbo la Catalunya Waislamu wanasalia nje na katika maeneo ya wazi kutokana na kutokuwa na maeneo ya ibada. 992872
captcha