IQNA

Saudia yafunga ubalozi wake nchini Misri

9:11 - April 29, 2012
Habari ID: 2313930
Serikali ya Saudi Arabia imetangaza kuwa imemwita nyumbani balozi wake mjini Cairo kwa ajili ya mashauriano na kwamba imefunga ubalozi huo na balozi nyingine ndogo nchini Misri.
Shirika la habari la Saudia limetangaza kuwa uamuzi huo wa kidiplomasia umechukuliwa kutokana na maandamano yanayoendelea kufanywa na wananchi wa Misri na majaribio ya kuvamia ubalozi huo.
Wananchi wa Misri wamekuwa wakifanya maandamano mbele ya ubalozi wa Saudia mjini Cairo wakilalamikia kutiwa nguvuni mwanaharakati wa masuala ya kisheria wa Misri nchini Saudi Arabia. Wanaharakati wa Kimisri wanasema mwanasheria Ahmad al Jizawi ametiwa nguvuni nchini Saudi Arabia kwa tuhuma za kumvunjia heshima mfalme wa nchi hiyo Abdullah bin Abdul Aziz baada ya kuwasilisha mashtaka mahakamani dhidi ya mfalme huyo kutokana na mateso na manyanyaso yanayofanywa na vyombo vya usalama vya serikali ya Riyadh dhidi ya raia wa Misri katika jela za Saudi Arabia.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaikosoa sana Saudi Arabia kutokana na mateso na manyanyaso wanayofanyiwa wafungwa katika jela za nchi hiyo. 995397


captcha