Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran aliyasema hayo Jumatano aliponana na maelfu ya walimu kutoka kila kona ya Iran.
Vile vile alizungumzia uchaguzi wa awamu ya pili ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na kusisitiza kwamba, siku ya Ijumaa (Mei 4, 2012) wananchi wa Iran watajitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi huo, ili kuonesha sifa yao bora na ya kupigiwa mfano ya kuwa macho, kuwa na muono wa mbali na kutambua vyema hali na mazingira yaliyopo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema katika mkutano huo uliofanyika katika siku za maadhimisho ya Siku ya Mwalimu nchini Iran na huku akitukuza nafasi na kumbukumbu za Ustadh Shahid Ayatullah Murtadha Mutahari na kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Mwalimu nchini amebainisha nafasi tukufu, ya juu na yenye thamani kubwa ya mwalimu na kuongeza kuwa, moja ya sifa muhimu kabisa ya mwalimu ni kwamba anakabidhiwa watu wenye vipaji, hisia, miguso na uwezo mkubwa wa masuala mbali mbali na kwamba jitihada na ubunifu wa mwalimu unaweza kuwafanya watoto na vijana anaokabidhiwa kuwa wasomi na wataalamu wakubwa na watu wema, wenye maarifa na uwezo mkubwa sana.
Ayatullah Udhma Khamenei amewausia watu wa matabaka mbali mbali, Wizara ya Elimu na Malezi nchini Iran na hata walimu wenyewe kwamba wajue thamani ya nafasi na heshima ya mwalimu na kusisitiza kuwa, kama mwalimu atatekeleza jukumu lake kwa njia sahihi, kwa umakini, kwa mapenzi na kwa kuwa na uchungu na kazi yake, basi bila ya shaka yoyote ataweza kuweka msingi madhubuti sana wa kuweza kuundwa jamii iliyo bora na kwa njia hiyo kuweza kutatua matatizo mengi ya kiutamaduni, kimaadili na kitabia ya jamii hiyo.
Vile vile ameashiria upande usio na mbadala wa Wizara ya Elimu na Malezi katika kila kona ya Iran bali hata katika maeneo ya mbali kabisa ya nchi hii na kusema kuwa, jukumu la wizara hiyo ni kubwa sana.
Vile vile amesema kuwa, katika miaka ya hivi karibuni kuna hatua nzuri zinazopaswa kupongezwa ambazo zimechukuliwa ndani ya Wizara ya Elimu na Malezi ya Iran huku muhimu kuliko yote ikiwa ni kuandaliwa hati ya mabadiliko ya kimsingi na kuongeza kuwa, ingawa hatua hiyo ni nzuri, lakini ujumbe muhimu na wa kimsingi uliopo hivi sasa ni kuhakikisha hati hiyo inatekelezwa kivitendo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, miongoni mwa mambo ya lazima katika utekelezaji wa hati ya mabadiliko ya kimsingi katika Wizara ya Elimu na Malezi nchini Iran ni kuwa na ratiba makini na ya kina na kuandaa ramani ya njia ya kuweza kufanikisha jambo hilo ili kwa njia hiyo kuweze kuainishwa njia ya kuweza kufikia malengo ya hati hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia umuhimu mkubwa na wa hali ya juu sana wa Wizara ya Elimu na Malezi nchini Iran na nafasi yake katika malezi sahihi ya vijana na katika kueneza maadili na tabia njema katika jamii na kuongeza kuwa, Wizara ya Elimu na Malezi nchini, inapaswa kuweka vigezo maalumu kwa ajili ya vijana na kwamba kigezo bora kabisa cha kuwawekea vijana hivi sasa ni vijana na mabarobaro waliokufa shahidi katika njia ya haki.
Ameongeza kuwa, inabidi tabia na sifa bora za mashahidi zikiwemo sifa za kuwa na ghera, hima, ukweli, kujitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu, kuwa na muono wa mbali na wa hali ya juu, mienendo mema na watu na pia mbele ya baba na mama na vile vile mbele ya marafiki zao zifundishwe na zipewe umuhimu mkubwa kwa vijana wa leo hii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha pia kuwa, mbali na Wizara ya Elimu na Malezi, taasisi nyinginezo za tablighi, Shirika la Televisheni na Redio la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali wakiwemo pia wanavyuoni wa kidini, wote wajue kuwa wana jukumu zito la kuwa vigezo, kuonesha mfano na kuunda vigezo bora vya kufuatwa katika jamii.
Ayatullah Udhma Khamenei pia ameashiria katika sehemu nyingine ya hotuba yake juu ya awamu ya pili ya uchaguzi wa tisa wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (yaani Bunge la Iran) na kusema kuwa, wananchi wa Iran wako macho wakati wote na kila inapolazimu huchukua hatua kwa wakati mwafaka ambapo mfano wa wazi wa jambo hilo ni jinsi wananchi wa Iran walivyojitokeza kwa wingi na kwa mwamko mkubwa katika awamu ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge iliyofanyika mwezi Esfand (Machi 2, 2012); na kwamba hatua ya wananchi wa Iran ya kuyajua vizuri mazingira na hali ya mambo ilivyo imeonyesha vizuri athari zake.
Vile vile ameashiria kutomalizika kazi na suala zima la uchaguzi wa tisa wa Bunge la Iran na kusisitiza kuwa, hatua ndefu na kubwa itakayopigwa na wananchi wa Iran katika siku ya Ijumaa ya tarehe 15 mwezi Ordibehesht (Mei 4, 2012), kwa kushiriki kwa wingi katika vituo vya kupigia kura na kumaliza kazi ya upigaji kura za Bunge la Tisa, kwa mara nyingine itawafanya wananchi hao wawaoneshe walimwengu jinsi wanavyotambua na kuijua vizuri hali na mazingira yaliyopo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia juu ya hali na mazingira yanayotawala duniani hivi sasa na kusema kwa kugogoteza kuwa, kama mataifa ya dunia yanataka kuwa na mafanikio basi hayana budi kuwa macho kikamilifu na kujitokeza wakati wote kwenye nyuga tofauti na kuonesha uwezo wako uwanjani.
Ameongeza kuwa, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu wananchi wa Iran wako uwanjani wakati wote, wana muono wa mbali na wanaijua vilivyo hali na mazingira yaliyopo kama ambavyo wanamjua vizuri adui yao na hawawezi kudanganywa na hila za adui za kujifanya kuwa ni rafiki kwa taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja uchaguzi kuwa ni moja ya madhihirisho ya kuweko uwanjani wananchi na kuongeza kuwa, taifa la Iran linapaswa kuwa macho uwanjani wakati wote ili liweze kulinda haki zake na haki za vizazi vyake vijavyo hususan kwa kuzingatia kuwa hivi sasa ulimwengu umetawaliwa na mazingira yaliyojaa mivutano kati ya madola ya kimaada na ya kupenda masuala ya kidunia.
Vile vile amesisitiza kuwa upeo wa mustakbali mwema uko wazi sana kwa ajili ya taifa la Iran na kuongeza kwamba, bila ya shaka yoyote kesho ya Iran ya Kiislamu ni bora zaidi kuliko leo yake kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Bw. Haji Babai, Waziri wa Elimu na Malezi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria suala la kupasishwa hati ya mabadiliko ya kimsingi kwenye wizara yake na kuongeza kuwa, kumeundwa makundi 12 ya wataalamu katika kituo kikuu na kamati 750 kote nchini Iran kwa ajili ya kuhakikisha kuwa hati hiyo inatekelezwa vile inavyotakiwa.
Vile vile ameashiria mabadiliko yaliyofanyika katika muundo wa Wizara ya Elimu na Malezi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongezwa nguvu za kitengo cha malezi akikutaja kuanzishwa kitengo maalumu cha afya za wanafunzi na elimu ya kujenga mwili, kuweka mipango ya kutekeleza mwamko wa taifa wa kuhifadhi Qur'ani Tukufu, kujenga kumbi elfu moja za michezo, kuweka mipango wa kuchunga na kusimamia matatizo na madhara yanayoikabili jamii, kukamilisha kazi ya kuvifikia vizuri zaidi kielimu vijiji vyote na kutoa mazingatio maalumu kwa wanafunzi bora na wenye vipaji, kuwa ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na wizara yake.
998684