IQNA

Maandamano ya kulaani uchomaji Qur'ani yafanyika Iraq

18:10 - May 05, 2012
Habari ID: 2318773
Wananchi wa Iraq siku ya Ijumaa walifanya maandamano makubwa mjini Baghdad kwa lengo la kulaani hatua mpya ya Kasisi Terry Jones ya kuchoma moto Qur'ani Tukufu.
Kwa mujibu wa tovuti ya As'watul Iraq, waandamanaji hao ambao kimsingi walikuwa wafuasi wa mrengo wa Muqtada Sadr wamelaani vikali kitendo cha kasisi huyo mwovu cha kuchoma tena Qur'ani na kisha kusambaza picha za kitendo hicho cha aibu kwenye mtandao wa intaneti.
Akizungumza katika maandamano hayo Sheikh Ahmad al-Ghaz-Ali mmoja wa wanazuoni wa Iraq amesema kwamba maandamano hayo yameitishwa kwa lengo la kulaani kitendo cha kasisi aliyetajwa wa Marekani na wito wake wa kutaka kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu kiendelee kuchomwa moto duniani, kama alama ya kudhihirisha chuki dhidi ya Uislamu. Amesema kitendo hicho kinatekelezwa na watu waovu kwa lengo la kuchochea fitina na mvutano kati ya mataifa ya dunia.
Watu walioshiriki kwenye maandamano hayo walitoa maoni tofauti na kueleza kuwa Kasisi Jones amefanya kitendo hicho cha dharau dhidi ya matukufu ya Kiislamu kutokana na chuki kubwa aliyonayo dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Wametaka kasisi huyo ahukumiwe katika mahakama za kimataifa, taasisi rasmi za serikali na mashirika yanayotetea haki za binadamu duniani, kwa sababu kinyume na anavyodai kasisi huyo, Qur'ani Tukufu ni kitabu kinachohubiri amani, upendo, huruma, ushirikiano, utu na udugu kati ya jamii ya wanadamu.
Maandaano kama hayo yamefanyika katika pembe tofauti za Iraq. 999936
captcha