IQNA

Imam Khamenei: Hijab inamletea heshima mwanamke

11:59 - May 14, 2012
Habari ID: 2325425
Husainia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ya mjini Tehran, imehinikiza anga ya umaanawi na nuru ya fadhila kubwa za Ahlul Bayt na "Kauthar" wa Mtume, kufuatia kufanyika katika Husainiya hiyo, maadhimisho ya kukumbuka siku ya kuzaliwa Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha), binti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW.
Husainia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ya mjini Tehran, imehinikiza anga ya umaanawi na nuru ya fadhila kubwa za Ahlul Bayt na "Kauthar" wa Mtume, kufuatia kufanyika katika Husainiya hiyo, maadhimisho ya kukumbuka siku ya kuzaliwa Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha), binti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran amehudhuria kwenye maadhimisho hayo na sambamba na kutoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa siku hiyo ya kihistoria na isiyoweza kusahaulika ya kuzaliwa Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha) na vile vile kutoa pongezi za kusadifiana siku hiyo na siku ya kukumbuka alipozaliwa Imam Khomeini (quddisa sirruh) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amezungumzia sifa mbali mbali maalumu katika maisha ya Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha) na amezitaja sifa hizo kuwa ni kigezo kamili cha kila upande cha fadhila na utukufu.
Aidha amekumbushia sababu za siku hiyo kupewa jina la Siku ya Mwanamke nchini Iran na huku akiashiri somo la kudumu milele wanalopata watu wote hususan wanawake na hasa akinamama wa Iran ya Kiislamu kutokana na maisha matukufu ya binti huyo wa Bwana Mtume Muhammad SAW, amewataka akinamama hao wajipambe kwa sifa za taqwa, staha, elimu, maarifa, ushujaa, kusimama kidete na kuwalea vizuri watoto wao ili kwa njia hiyo waweze kuzifanya familia zao ziingie katika mkondo wa maisha ya Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha).
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia uhakika usiopingika kwamba akili na ulimi wa mwananaadamu unakosa maneno ya kubainisha fadhila na utukufu na adhama ya binti huyo mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW na kuongeza kuwa, pamoja na kwamba huo ndio uhakika wa mambo, lakini miongozo, maneno na maisha ya Bibi huyo mtukufu na Maimamu wengine watoharifu yamo mikononi mwa mwanaadamu, bali tofauti na watu ambao leo hii wanafanywa vigezo duniani licha ya kwamba hawana sifa zozote za kuwa vigezo vizuri vya kufuatwa, kwa upande wa Maimamu watoharifu (Alayhimus Salaam) ni kuwa wanaonesha njia na sirati sahihi kwa ajili ya kufanyika harakati na kuendesha maisha yao watu wote huku Maimamu hao watukufu wakiongoza na kuwa juu kabisa ya vilele vya ukamilifu huo wa kibinaadamu sambamba na kuwalingania watu kufuata njia hiyo ya uwokovu wa kweli.
Vile vile amezitaka jamii zote na hasa akinamama, kufuata njia ya utukufu wa kimaanawi wa Maimamu watoharifu na huku akiashiria historia ya mapambano ya wanawake wa Kiirani katika nyuga tofauti kuanzia mapambano ya zama za kupigania mfumo wa Katiba nchini Iran hadi kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na katika kipindi chote cha vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran ameongeza kuwa, uwepo huo wenye taathira kubwa wa wanawake wa Kiirani katika nyuga hizo ulifanyika huku wanawake hao wakiwa wanalinda na kuheshimu kikamilifu vazi la staha la Hijabu na kwamba jambo hilo linaonesha kuwa wanawake wanaotunza Hijabu wanaweza kushiriki vilivyo katika nyuga hizo na kutimiza majukumu yao kwa ushujaa mkubwa. Amewataja mama wa mashahidi nchini Iran kuwa ni mfano wa wazi kabisa wa jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei pia ameashiria njama zinazofanywa na maadui za kuupa nguvu udhaifu unaojitokeza hapa na pale katika umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa, mwanaadamu leo hii anakabiliwa na hatari kubwa na anapaswa kuwa macho katika matendo yake na inabidi tujue kuwa baadhi ya madhihirisho ya kujionyesha wazi wazi wanaokhalifu mafundisho ya Mwenyezi Mungu, kutokuwa na taqwa na kutochunga Hijabu na staha, yana athari mbaya na za muda mrefu katika maadili, "Akhlaqi" na siasa za jamii, na kwamba wanawake ndio wanaopaswa kuwa macho zaidi na kuchunga vilivyo mambo yao katika jambo hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja vazi la staha la Hijabu kuwa linampa mwanamke heshima yake na ni sababu ya kupata utulivu na hadhi yake na kubainisha kwamba, staha ya wanawake hupelekea kupatikana fakhari, kuzidi kupata heshima, na kuzidi kupata nguvu hadhi na manzili ya mwanamke katika jamii. Amesema, ni kwa sababu hiyo ndio maana inabidi tuishukuru sana dini tukufu ya Kiislamu kutokana na kuzingatia vilivyo suala la kuchungwa vazi la staha la Hijabu katika jamii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwamba elimu na maarifa ya Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kusisitiza kuwa, hatua ya Ahlul Bayt AS ya kumshukuru Mwenyezi Mungu katika kalibu ya tungo za kishairi na nathari ni neema nyingine na amewataka watu wanaosoma kasida za Ahlul Bayt wajue thamani ya kuwa na urithi mtukufu kama huo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia kuwa, kutangaza fadhila na utukufu wa kimaanawi wa Ahlul Bayt (Alayhimus Salaam) kunazidi kuipelekea jamii iwafanye watukufu hao vigezo vyao vizuri na kuongeza kuwa, kama harakati hiyo itafanyika katika jamii kwa ikhlasi na kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, basi bila ya shaka yoyote itakuwa na matunda mazuri sana. Hivyo amewataka watu wanaosoma kasida za Ahlul Bayt AS waangalie kwa kina ni miongozo gani ya watukufu hao ambayo itaweza kuwaongoza walengwa na kuongeza unyenyekevu na khushuu katika nyoyo za wasikilizaji wao mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuwafanya wasikilizaji wao hao wapate hamu ya kuingia katika njia tukufu ya Ahlul Bayt AS.
Amesema, kazi ya jamii ya watu wanaosoma kasida za Ahlul Bayt (Alayhimus Salaam) ni kubainisha uhakika kupitia sauti zao nzuri na za kuvutia ndani ya tungo zenye mnato na athari kubwa katika nyoyo za wasikilizaji na kuongeza kuwa, kutumia vizuri mbinu mbali mbali za kisanii katika kutangaza uhakika huo bila ya shaka yoyote kuna faida na athari kubwa kwa mlengwa, hivyo inabidi jambo hilo lifanyiwe kazi, lisomeshwe na liwe la kifikra.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia upeo wa hali ya juu wa ufahamu, maarifa, kina cha hali ya juu cha kifikra, tabasuri, muono wa mbali na mtazamo wa kina wa jamii na kuongeza kuwa, leo hii uwezo wa Iran ya Kiislamu katika nyuga tofauti unameremeta na kung'ara katika kila kona ya ulimwengu huu wa kimaada na unatoa mwangaza mithili ya jua. Pia amewataka wasomaji wa kasida za Ahlul Bayt nao wajuwe kuwa wanapaswa kuizingatia anga hiyo inayotawala hivi sasa na kutunga tungo zenye maana nzito na faida kubwa kwa ajili ya wasikilizaji wao.
Mwanzoni mwa mkutano huo, wasomaji kadhaa wa mashairi na kasida za Ahlul Bayt (Alayhimus Salaam) wamesoma kasida zao mbele ya Kiongozi Muadhamu zilizohusiana na heshima na utukufu wa binti wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha) pamoja na mashairi ya kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Khomeini (quddisa sirruh) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.


1006278
captcha