Jameel Kadhim Katibu Mkuu wa Mrengo wa Kiislamu wa al Wifaq aliyasema hayo hapo jana katika mahojiano na televisheni ya Al Alam na kuongeza kuwa, dalili zinaonyesha kuwa nchi mbili yaani Saudi Arabia na Bahrain zinakusudia kuanzisha muungano na kwamba hatua hiyo katu haitaweza kusimamisha harakati za mapinduzi za wananchi wa Bahrain. Ameongeza kuwa, malengo ya utawala wa Aal Khalifa katika kuanzisha muungano huo ni kupata wasaa wa misada kutoka kwa nchi wanachama wa Baraza la ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kwa ajili ya kufuta mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo.
Kuufahamu mwamko wa Bahrain
Kwa hivyo kwa kufahamu aina ya utawala wa Bahrain, tunaweza kufahamu sababu za mwamko wa Wabahrain.
Bahrain ni nchi inayojumuisha visiwa kadhaa vidogo na mfumo wake wa utawala ni wa kurithiana kiti cha ufalme baina ya ukoo wa Aal Khalifa. Aidha nafasi zote muhimu serikalini zimenyakuliwa na watu wa ukoo wa Aal Khalifa ambao huteuliwa na Mfalme Hamad bin Isah Aal Khalifa kushikilia nyadhifa hizo.
Utawala wa Bahrain una mabunge mawili yaani baraza la juu na baraza la chini ambapo wajumbe wa baraza la juu huchaguliwa na mfalme.
Kimsingi ni kuwa nchini Bahrain, wananchi hawana nafasi yoyote katika kuainisha viongozi na uchukuzi wa maamuzi muhimu. Uteuzi na ufutaji wa watu wanaoshikilia nafasi zote muhimu hutekelezwa na mfalme na yeye ndiye mwenye kauli ya mwisho katika masuala yote muhimu.
Wananchi wa Bahrain hawana imani hata kidogo na mfalme wa sasa wa nchi hiyo Hamad bin Isah Aal Khalifa na kwa hivyo ili kuendeleza utawala wake, mfalme huyo ameamua kutegemea utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na Marekani.
Utegemezi wa Bahrain kwa Saudi Arabia ni mkubwa kiasi kwamba mahitajio karibu yote ya kawi na nishati ya Bahrain hudhaminiwa na Saudi Arabia. Aidha nchi hizi mbili za Ghuba ya Uajemi zinaunganishwa pamoja kupitia daraja lenye urefu wa kilomita 25.
Aal Khalifa anategemea Marekani kubakia madarakani
Katika upande mwingine, mfalme wa Bahrain ni kati ya waungaji mkono wakubwa wa Marekani katika eneo na kutokana na hilo Bahrain ni kituo kikuu cha 'Msafara wa Tano wa Manuari za Jeshi la Majini la Marekani'. Kituo hicho cha jeshi la wanamaji Marekani kinashughulikia vikosi vya jeshi la wanamaji la Marekani katika Ghuba ya Uajemi, Bahari Nyekundu, Bahari Arabu na Pwani ya Afrika Mashariki. Kwa hivyo kwa kutegemea uungaji mkono wa Marekani na Saudi Arabia, mfalme wa Bahrain amewanyima wananchi uhuru na haki yao ya kuainisha mstakabli wa nchi yao.
Moja ya sababu muhimu zaidi za mwamko wa watu wa Bahrain dhidi ya hali iliyopo ni utegemezi wa Mfalme Hamad bin Isah Aal Khalifa kwa serikali ya kibeberu ya Marekani.
Tovuti ya intaneti ya chama cha upinzani cha Al Wifaq ambacho ndicho chama muhimu zaidi cha kisiasa Bahrain imeandika hivi kuhusu utegemezi wa ukoo wa Aal Khalifa: "Mwamko wa watu wa Bahrain pamoja na kuwa unashabihiana na miamko katika maeneo mengine lakini una nukta ya kipekee ambayo ni chimbuko lake. Bahrain ni kituo cha kijasusi, kijeshi na kisiasa cha Marekani. Serikali ya nchi hii haina sifa zozote za demokrasia.' Chama cha Al Wifaq kimeongeza kuwa: 'Nchi hii sasa ni kituo cha kijeshi cha Marekani na mahala pa kustarehe maafisa wa jeshi la Marekani. Wasaudi nao pia kila mwisho wa wiki kupitia daraja, huingia Bahrain kustarehe na hivyo utawala wa Aal Khalifa hauhitajii wananchi wake. Kimsingi ni kuwa utawala wa Bahrain unategemea raia wa kigeni katika jeshi na vyombo vya usalama. Raia hao wa kigeni hatimaye hupewa uraia wa Bahrain.' Kwa hivyo kubadilishwa Bahrain kuwa kituo cha kijeshi cha Marekani ni moja ya sababu ambazo zimepelekea Wabahrain kukasirika na kuandamana mitaani. Watu wa Bahrain wanataka mfumo wa kidemokrasia ili waweze kuwa huru pasina kutegemea madola ya kigeni.
Katika upande mwingine, Marekani inatumia uwezo wake wote kuupa himaya utawala wa kifalme wa Bahrain na hata Washington imempa mfalme Hamad Aal Khalifa silaha za kuwakandamiza wananchi wanaoandamana kwa amani. Kwa hivyo kinachobainika wazi hapa ni kuwa nara za kutetea haki za binaadamu zinazotolewa na watawala wa Marekani na Ulaya ni uongo mtupu. Wamagharibi wameonyesha undumakuwili wao kwa kuunga mkono utawala dhalimu na wa kiimla wa Bahrain.
Marekani inataka utawala wa kiimla ubakie Bahrain
Henry Kissinger waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani anaweka nukta hiyo wazi kwa kukiri kuwa: 'Mabadiliko ya kuleta demokrasia Bahrain hayatadhamini maslahi ya Marekani. Waislamu Mashia wakichukua mamlaka Bahrain, jambo hilo litakuwa ni kinyume kabisa na maslahi ya Marekani. Aidha mbali na maslahi ya Marekani, maslahi ya Saudi Arabia pia yatakuwa hatarini. Ni kwa sababu hii ndio Marekani ikafanya kila iwezalo kuulinda na kuuhifadhi utawala wa Aal Khalifa na Saudia nayo imeungana na Marekani katika hili'.
Njama ya vyombo vya habari dhidi ya watu wa Bahrain
Moja ya hatua ambazo zimechukuliwa na vyombo vya habari vya Kimagharibi na Kiarabu ni kutotangaza habari za Bahrain na hasa kuficha habari kuhusu ukatili, udhalimu na ukandamizaji wa utawala wa Aal Khalifa dhidi ya wananchi wanaoandamana kwa amani.
Ukandamizaji wa kikatili Bahrain na jinsi vyombo vya habari hasa vya Kimagharibi vinavyoakisi habari za matukio ya nchi hiyo ni mfano wazi wa ubanaji habari za kweli. Noam Chomsky mwanafikra wa Kimarekani amejadili suala hili la kukosa kuakisiwa habari kuhusu matukio ya Bahrain na kusema hilo si jambo jipya kwani kuna mifano ya huko nyuma ya kuficha habari za kweli katika vyombo vya habari vya Kimagharibi.
Nchi za Kiarabu nazo zinajaribu kupotosha ukweli kuhusu habari za Bahrain. Kuhusiana na hili nafasi ya kanali ya televisheni ya utawala wa Qatar ya Al Jazeera na utegemezi wake kwa sera za nchi za Magharibi ni jambo lililowazi kabisa.
Al Jazzera, Al Arabiya zaficha ukweli
Katika hali ambayo Al Jazeera kidhahiri iliunga mkono harakati za wananchi katika mapinduzi yaliyojiri katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika lakini kanali hiyo imeonyesha udhaifu mkubwa katika kuakisi ukweli wa mambo katika matukio ya Bahrain. Nayo kanali ya televisheni ya Al Arabiya inayomilikiwa na watawala wa Saudi Arabia ni kati ya kanali ambazo zimebana sana ukweli kuhusu harakati ya kutetea haki ya watu wanaodhulumiwa Bahrain. Al Arabiya imeficha kabisa udhalimu wa Aal Khalifa na Aal Saud na hasa wa kufungwa jela waandamanji bila kusikilizwa kesi zao, utesaji na unyanyasaji pamoja na matukio mengine mengi kuhusu mwamko wa watu wa Bahrain.
Bahrain si tu kuwa ni tegemezi kwa vikosi vya kigeni bali hata wafanyakazi wake wa kawaida ni kutoka nchi kama vile Ufilipino, Bangladesh, Sri Lanka na nchi zinginezo za kusini mwa Asia. Hii ni katika hali ambayo kuna raia wengi asili wa Bahrain ambao hawana ajira jambo ambalo linaonyesha kuwa utawala wa kifalme umekataa makusudi kutekeleza jukumu lake la kuwapa Wabahraini nafasi za kazi. Fauka ya hayo, utawala wa kiimla wa Aal Khalifa unawachukua mamluki wa kigeni ambao aghalabu wanazungumza vizuri lugha ya Kiarabu na kuwatumia katika kuwakandamiza na kuwatesa wananchi wanaoandamana. Ikumbukwe kuwa vyama vyote vya kisiasa vimewataka wananchi waandamane kwa amani pasina kutumia silaha.
Maandamano ya amani yavunjwa kwa mtutu wa bunduki
Katika kufuata mwito huo wananchi wanaodhulumiwa Bahrain wanaadamana kwa amani na hadi sasa hawajachukua silaha dhidi ya wanajeshi wa ukoo wa Aal Khalifa wala wanajeshi vamizi wa Saudi Arabia. Lakini wanajeshi wa utawala wa kifalme wanawakandamiza wananchi kwa kutumia vifaru, mtutu wa bunduku na gesi ya kutoa machozi yenye kemikali za sumu. Hivi sasa kusimama kidete watu wa Bahrain kumeonyesha kuwa mwamko hauwezi kuzimwa kwa ukandamizaji, na hii ndiyo nukta muhimu katika mwamko wa watu wa Bahrain. Kile ambacho wananchi wanamapinduzi wa Bahrain wanataka ni kuanzishwa mfumo wa serikali uliojengeka katika msingi wa kura na kushirikishwa wananchi wote. Aidha wanataka Bahrain iwe huru kikamilifu na isiwe tegemezi kwa nchi za Magharibi.
Moja ya sifa nyingine za mwamko wa watu wa Bahrain ni mshikamano na umoja wa watu wa makabila na madhehebu yote nchini humo. Pamoja na kuwa Mashia ndio wengi zaidi katika jamii ya watu wa Bahrain lakini wananyimwa haki zao za kimsingi na utawala wa Aal Khalifa unazidi kuwadhulumu. Maeneo yenye wakaazi wengi wa Kishia Bahrain yamezama katika umasikini na yamesahaulika kabisa katika mipango ya maendeleo. Aidha katika maeneo ya Mashia idadi ya watu wasiokuwa na kazi ni kubwa sana. Masuala hayo yamepelekea wapinzani wa mwamko wa watu wa Bahrain kudai kuwa mwamko huo ni wa Mashia pekee katika hali ambayo hakuna ukweli wowote katika madai hayo.
Masunni na Mashia Bahrain waungana kuitisha mabadiliko
Matakwa ya watu wa Bahrain hayako katika fremu ya masuala ya kimadhehebu au kikabila bali watu wote wa Bahrain wakiwemo Mashia na Masunni kwa mashikamano wanataka kufikia lengo la pamoja. Wabahraini wote wanataka marekebisho ya mfumo wa utawala na kisiasa na mabadiliko ya kimsingi yatakayopelekea kuondolewa dhulma na ukosefu wa uadilifu katika jamii. Hivi sasa pamoja na mauaji , kufungwa waanndamanaji, mateso, kufutwa kazi waandamannaji na jinai zingine zote zinazotekelezwa na vikosi vya utawala wa Aal Khalifa kwa himaya ya Saudi Arabia dhidi ya taifa la Bahrain, lakini bado watu wa Bahrain wangali na moyo imara wa mapambano na wameazimia kuendeleza mapambano yao. Kuendelea mwamko wa watu wote wa Bahrain kunatokana na istikama na kusimama kidete wananchi hao wanaodhulumiwa. Kwa hakika kusimama kidete na mashikamano ni nukta muhimu katika mwamko wa watu wa Bahrain jambo ambalo limpelekea utawala wa Aal Khalifa kuchanganyikiwa. Inaelekea kuwa hatua za kimabavu kama vile kuwatia nguvuni wanamapambano, kuwafuta kazi wafanyakazi wapinzani na kuwatimua wanafunzi na hatua zinginezo zinazochukuliwa na utawala dhalimu wa Aal Khalifa, badala ya kudhoofisha wananchi zimezidisha irada imara ya waandamanaji na kuzidisha hisia za chuki dhidi ya watawala.
Taifa la Bahrain, kwa taufiki ya Allah, litapata ushindi
Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema hivi kuhusu kudhulumika mwamko wa watu wa Bahrain: 'Tab'an baina ya mataifa (yaliyo katika mwamko), taifa la Bahrain limedhulumika zaidi ya yote. Hii ni kwa sababu, katika hatua ya kusikitisha, mwamko huo umesusiwa na vyombo vya habari duniani. Hakuna mantiki yoyote ya kibinaadamu na kidunia inayopinga wanayotaka watu wa Bahrain. Matakwa ya Wabahrain ni ya haki lakini wamedhulimiwa. Kwa ujumla Wabahrain wameondolewa katika propaganda za kawaida za kihabari bali hata kunaenezwa propaganda dhidi yao. Tab'an hilo halina athari. Taifa la Bahrain, kwa taufiki ya Allah, litapata ushindi.'
1006997