Kwa upande wa kura zilizopigwa nje ya nchi wagombea wenye mielekeo ya Kiislamu wamejipatia kura nyingi zaidi katika vituo vingi. Hata hivyo nukta muhimu zaidi kuhusiana na zoezi la upigaji kura wa Wamisri waishio nje ya nchi ni kwamba japokuwa watu 587,000 walikuwa wametimiza masharti ya kupiga kura lakini ripoti zinaonyesha kuwa idadi ya watu walioshiriki katika zoezi hilo ni chini ya laki moja, na kati ya waliopiga kura wengi wao ni wale waishio nchini Saudi Arabia.
Wakati huo huo huku zikiwa zimesalia siku tatu tu kabla ya kufanyika uchaguzi wa kwanza wa rais nchini Misri tangu dikteta Hosni Mubarak alipong'olewa madarakani kampeni za wagombea zingali zinaendelea huku zikizidi kupamba moto. Ahmad Shafiq, ambaye ni mgombea mwenye misimamo ya kiliberali amepopolewa kwa viatu na mmoja wa hadhirina katika mkutano wa kampeni uliofanyika huko Aswan. Japokuwa wafuasi wake walimtia mbaroni haraka mtu huyo na kujaribu kutuliza hali ya mambo kwa kutoa kaulimbiu za kumuunga mkono Shafiq, lakini mkanda wa tukio hilo ulisambaa haraka kwenye mtandao wa intaneti. Aidha katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la al Watan linalochapishwa nchini Saudia Ahmad Shafiq amesema ataupa umuhimu mkubwa uhusiano wa nchi hiyo na Misri. Mgombea huyo anayeungwa mkono na Baraza Kuu la Kijeshi linaolotawala Misri hivi sasa aidha amesisitiza kwamba Cairo itaendelea kuheshimu makubaliano na mikataba yake yote ya kimataifa ukiwemo wa Camp David iliosaini na utawala wa Kizayuni wa Isarel, hata hivyo atajaribu kuvifanyia marekebisho baadhi ya vipengee vya mkataba huo hususan vile vinavyohusiana na eneo la Sinai. Katika upande mwengine wanaharakati na wafuasi wa Muhammad Mursi, mgombea wa chama cha Uhuru na Uadilifu (FJP) ambalo ni tawi la kisiasa la harakati ya Ikhwanul Muslimin, siku ya Alkhamisi walitengeza mnyororo mkubwa wa safu za watu katika mji mkuu Cairo, na huku wakiwa wamebeba picha za Mursi walipiga nara na sha'ar za kumuunga mkono mgombea huyo. Wakati huo huo uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni kabisa umeonyesha kuwa Abdul Mun'im Abulfutuh, mwanachama wa zamani wa Ikhwanul Muslimin, Amr Moussa, Katibu Mkuu wa zamani wa Arab League na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Misri pamoja na mgombea wa Ikhwanul Muslimin Muhammad Mursi ndio wanaoongoza kwa utaratibu katika nafasi tatu za mwanzo. Uchaguzi wa rais wa Misri utafanyika siku za Jumanne na Jumatano wiki hii na endapo hakutokuwa na mgombea atakayepata kura za kumwezesha kutangazwa mshindi, duru ya pili ya uchaguzi huo itafanyika tarehe 16 na 17 za mwezi ujao wa Juni.
1011140