Essam Al Uryan mmoja kati ya viongozi wa Chama cha Uhuru na Uadilifu kinachofungamana na Harakati ya Ikwanul Muslimin amesema kuwa: 'Kamwe hatutaruhusu utawala wa Mubarak urejee tena na tutaikata mikono ya watu wanaofuatilai lengo kama hilo.
Huku zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa Rais wa Misri likielekea ukingoni, matokeo yanaonesha kuwa hadi sasa mgombea wa harakati ya Ikhwanul Muslimn anaongoza katika uchaguzi huo.
Kundi la Ikhwanul Muslimin limetangaza kwamba baada ya kuhesabiwa asilimia 90 ya kura katika mikoa tofauti ya Misri, Muhammad Morsi mgombea wa chama cha Usawa na Uadilifu ambacho ni tawi la kisiasa la harakati hiyo anaongoza kwenye kinyang'anyiro hicho.
Matokeo hayo pia yanaonyesha kwamba Ahmed Shafiq, Waziri Mkuu wa mwisho wa utawala wa dikteta Hosni Mubarak uliopinduliwa na wananchi nchini humo anashika nafasi ya pili na wagombea wengine wakifuata nyuma.
Wagombea hao wawili ndio wanaotarajiwa kuingia katika duru ya pili ya uchaguzi wa Rais wa Misri utakaofanyika tarehe 16 na 17 mwezi ujao wa Juni. Muhammad ash Shahabi, mmoja wa mawakala wa tume ya uchaguzi ya mgombea wa kujitegemea Abdul Mun'im Abul Futuh amegusia baadhi ya mambo yaliyovunja waziwazi sheria za uchaguzi akisema kuwa, kununua kura za wananchi kulikofanywa na wagombea wanaouunga mkono utawala wa zamani wa nchi hiyo kulikuwa wazi kiasi kwamba katika saa za awali za upigaji kura, wagombea hao walikuwa wakinunua kila kura ya mtu kwa Pauni 200 za Misri na ilipofika masaa ya mwisho ya kupiga kura, walipandisha bei na kufikia hadi Pauni 500 kwa kila kura. Alaakullihaal, uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia wa rais umefanyika nchini Misri na taifa hilo la Kiislamu hivi sasa linasubiri matokeo ya uchaguzi huo. Wachambuzi wa mambo wanawatabiria ushindi wagombea wa mirengo ya Kiislamu hasa kwa vile chaguzi zilizotangulia za Bunge ziliwapa ushindi mkubwa wagombea wa mirengo hiyo. Tab'an suala la kuwa na maisha bora, utulivu, usalama na ustawi wa kijamii ni miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa na wapiga kura. Kuna uwezekano pia wa kuingia uchaguzi huo katika duru ya pili na hii ni kwa sababu kwa mujibu wa sheria za uchaguzi wa Misri, mgombea anapaswa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika duru ya kwanza na kama hilo litashindikana, basi uchaguzi huingia katika duru ya pili. Si hayo tu, lakini pia uvumi kwamba kuna uwezekano wanajeshi wanaotawala Misri hivi sasa wakachakachua matokeo ya uchaguzi huo, nao umepata soko kubwa kiasi kwamba wananchi wana wasiwasi juu ya hatari ya kutiwa mkono matokeo ya uchguzi huo. Alaakullilhaal, lililobakia hivi sasa ni kusubiri na kuona zoezi la kuhesabu kura litakuja na kitu gani huko nchini Misri.
1016403