Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International limesema katika ripoti yake ya mwaka huu wa 2012 kwamba utawala wa Saudi Arabia unakandamiza bila huruma maandamano ya amani yanayofanywa na raia wa nchi hiyo na hasa katika maeneo yenye wakaazi wengi wa Kishia mashariki mwa nchi hiyo.
Ripoti hiyo inasema kuwa utawala wa Saudia umekuwa ukikandamiza, kutesa na kuwafunga jela kidhulma mamia ya waandamanaji wanaoandamana kwa amani kwa lengo la kupigania haki zao za kimsingi. Imesema wengi wa wafungwa hao ni Mashia walioshiriki katika maandamano ya amani ya mwaka uliopita wa 2011 na pia wanaharakati wa kueteta haki za wanawake. Imeendelea kusema kuwa maelfu ya Mashia wengine wamefungwa jela kwa sababu zisizofahamika vyema kuhusiana na masuala ya kiusalama. Imesema mateso na vifungo vya kidhulma vya muda mrefu kwa Mashia ni jambo la kawaida kabisa nchini Saudia. Imeendelea kusema kuwa vifungo hivyo huandamana na vitendo vya kinyama, dharau na uvunjiwaji heshima wafungwa. Ripoti hiyo inasema kwamba sheria za Saudi Arabia zinaruhusu mabinti na wanawake kubaguliwa na kufanyiwa vitendo vya mabavu na kwamba wanaolalamikia hali hiyo hukamatwa na kufungwa jela. Amnesty International imesema kuwa wafanyakazi wengi wa kigeni wanaofanya kazi nchini humo huteswa na kutumiwa vibaya na waajiri wao lakini kwamba wahalifu hao huwa hawafikishwi mbele ya vyombo vya sheria kujibu mashtaka kuhusu suala hilo. Ripoti hiyo pia imeashiria kwamba mwaka huu pekee watu 82 tayari wamekwishanyongwa nchini humo idadi inayoonyesha kwamba kiwango cha kunyongwa watu nchini humo kimeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. 1016759