IQNA

Mwamko wa 15 Khordad, nukta muhimu katika Harakati ya Imam Khomeini MA

14:52 - June 02, 2012
Habari ID: 2339349
Kila harakati na mapinduzi huwa na nukta ya kuanzia. Cheche asili ya Mapinduzi ya Kiislamu Iran ilikuwa miaka 15 kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mnamo Juni tatu mwaka 1963.
Hata kama harakati ya mwamko ya Imam Khomeini MA ilikuwa imeanza huko nyuma, lakini mwamko ulioandamana na umwagikaji wa damu ya watu wa Iran ulianza katika msimu wa joto wa mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka 63 dhidi ya mfumo wa kidikteta wa Shah. Hapo ndipo Imam Khomeini alipotajwa kuwa kiongozi wa Mamko wa Kiislamu Iran.
Katika maisha yaliyojaa hamasa na mapambano ya Imam Khomeini dhidi ya utawala wa kiimla wa kifalme, tarehe 15 Khordad mwaka 1342 Hijria Shamsia, sawia na tarehe tatu Juni mwaka 1963, ilikuwa tarehe muhimu kiasi kwamba Imam alisema Mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa ni kuendeleza mwamko wa 15 Khordad. Karibuni kusikiliza kipindi hiki tulichowaandalia kwa mnasaba huu.

Mwamko huu ulikuwa mapambano yaliyojengekeza katika misingi mitatu ya Uislamu, Imam Khomeini na Wananchi. Mwamko huu ulipewa lakabu ya siku ya Hijria ya Shamsia ya kuanza kwake yaani Mwamko wa 15 Khordad. Mwamkoo huu ulikandamizwa vikali, na mwaka mmoja baada ya kuanza kwake, Imam Khomeini MA alibaidishwa Uturuki na kisha Iraq. Pamoja na hayo mwamko ulishika kasi na Maulamaa wa Kiislamu Iran wakaendeleza mapambano dhidi ya utawala wa kiimla wa Mohammad Reza Pahlavi na waitifaki wake Wamarekani.
Kile ambacho kilipelekea kuibuka mwamko wa 15 Khordad mwaka 1963 ni matukio yaliyojiri nje ya Iran. Uchaguzi wa rais mwaka 1960 nchini Marekani ulipelekea kuchaguliwa John F Kennedy wa chama cha Democrat na hivyo kusababisha mabadiliko katika sera za kigeni za Marekani. Kuleta madarakani serikali zisizo za kijeshi na ambazo ni vibaraka wa Marekani ni kati ya sera zilizofuatiliwa kwa karibu na serikali ya Kennedy. Mohamad Reza, Mfalme wa Iran katika wakati huo aligeuka na kuwa kibaraka mkubwa wa Marekani. Alinyakua madaraka baada ya mapinduzi ya serikali ya Iran yaliyotekelezwa na Marekani kwa ushirikiano na Uingereza mwaka 1953 na kupelekea kuanguka serikali ya kitaifa ya Dkt. Mossadeq.
Ili kuendeleza utawala wake, Mohammad Reza hakuwa na budi ila kuiridhisha Marekani kwa kutekeleza mabadiliko ya kidhahiri ya kisiasa nchini. Mabadiliko hayo yalipewa jina la ‘Mapinduzi Meupe’ na yalikuwa na lengo ya kuupiga vita Uislamu na badala yake kurundika utamaduni wa Kimagharibi Iran. Imam Khomeini aliwatangazia wananchi hatari iliyokuwepo kutokana na sera za Shah za kuupiga vita Uislamu.
Hotuba zilizotolewa na Imam Khomeini MA zilipelekea kuibuka maandamano ya wananchi waliopinga sera hizo za Shah. Katika kukabiliana na hali hii, Shah alitumia vikosi vyake kushambulia Chuo cha Faiziya cha Qum na hasa wanazuoni na wanafunzi wa kidini ili kukandamiza malalamiko yaliyokuwepo. Lakini ukandamizaji huu ulizidisha malalamiko ya wananchi dhidi ya Shah. Maandamano ya kidini na nara za kimapinduzi dhidi ya utawala wa Shah na uungaji mkono wa wananchi kwa harakati ya Imam Khomeini yaliyoanzia Qum yalienea hadi Tehran na maeneo mengine ya Iran. Kutokana na kupanuka wigo wa maandamano, utawala wa Shah uliona njia bora zaidi ya kuendeleza sera zake dhidi ya Uislamu ni kwa kumtia nguvuni Imam Khomeini. Habari za kutiwa mbaroni Imam Khomeini zilipelekea maandamano kushadidi katika maeneo yote ya Iran. Hali ya hatari ilitangazwa Qum, Tehran na miji mingine nchini. Katika kukabiliana na waandamanaji, maafisa wa usalama wa Shah waliwaua mamia ya watu na kuwatia mbaroni maelfu ya wengine. Utawala wa Shah ulidhani kwa kumtia nguvuni Imam na wafuasi wake, hatua hiyo ingeweza kuzima mwamko wa 15 Khordad.
Hii ni katika hali ambayo Imam hakubadilisha msimamo wake hata kidogo wala umashuhuri wake haukupungua na wananchi walibaki katika medani za maandamano. Hotuba za Imam zilifichua ufisadi wa utawala wa Shah. Wananchi walimkubali Imam kama kiongozi wa harakati ya mwamko. Ingawa harakati ambayo Imam Khomeini alikuwa akiiongoza kutokea Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum ilikandamizwa na utawala wa kifalme lakini haikuzimika. Harakati hiyo iliendelea chini kwa chini na kisha baada ya miaka 15, yaani Februari mwaka 1979, ilipata ushindi mkubwa na hivyo kuangamiza kabisa utawala wa kiimla wa kifalme nchini Iran.
Miaka kadhaa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini alifafanua mwamko wa 15 Khordad kwa kusema: “Mwamko wa tarehe 15 Khordad uliakisi ukweli kuwa, iwapo taifa litahujumiwa na kutekwa na kundi la madikteta wanaotumia mabavu na wapendao madaraka, ni irada ya taifa tu ndiyo inayoweza kusimama kidete kukabiliana na dhulma ili kuainisha hatima yake. 15 Khordad ilikuwa siku yenye baraka na hata kama damu takasifu ya vijana ilimwagika katika ardhi hii lakini huo ulikuwa mwanzo wa harakati kubwa katika uga wa uhai wa kisiasa na kijamii katika jamii.”

Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliongeza: “Kile kilichokuwa na umuhimu katika mwamko wa 15 Khordad ni kuvunja haiba iliyooza na utawala kibaraka wa kifalme ambao ulikuwa na ndoto ya kuvuruga mwamko lakini tuliona namna harakati ya pamoja iliyoandamana na umoja na maelewano ya kitaifa yalivyopelekea adhama yote ya utawala wa kifalme kusambaratika mara moja.”

Mwamko wa 15 Khordad uliweka wazi mpaka baina ya harakati ya Kiislamu iliyokuwa ikipambana dhidi ya Shah na harakati zingine za kisiasa zilizodai kupambana na utawala huo.
Mwamko wa 15 Khordad ulikuwa mwanzo wa harakati ya watu wa Iran na mwamko huu ulikuwa wa Kiislamu mia kwa mia. Kutokana na utambulisho wake wa Kiislamu, mwamko huu ulijitokeza chini ya uongozi wa shakhsia ambaye alikuwa Marja’a Taqlid na Faqihi katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum.
Kwa uongozi wa Imam Khomeini, njama ya kutenganisha dini na siasa ilivunjwa. Utawala wa kiimla wa Shah kwa miaka mingi ulikuwa ukieneza propaganda potofu za kutenganisha siasa na dini. Wananchi Waislamu wa Iran walianzisha mapambano ya Kiislamu ambayo waliyachukulia kuwa wajibu wao wa kidini kama swala na saumu. Idiolojia na mafunzo ya mwamko huu yalikuwa ya Kiislamu na misingi yake ilitokana na Qur’ani pamoja na Sunnah ya Mtume SAW na Ahlul Bayt wake AS.
Sifa ya pili ya kipekee ya harakati ya mwamako wa 15 ni kudhihirika kikamilifu nafasi ya Imam Khomeini kama kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya kupambana dhidi ya utawala wa Shah,
Uongozi wa Imam, uliondoa kabisa dhana potofu ya kutenganisha dini na siasa. Motisha wa Imam Khomeini katika kupambana dhidi ya utawala wa Shah haukushabihiana hata kidogo na motisha wa wanamapambano wa mrengo wa kushoto au wapinga ubeberu wasio kuwa na dini. Mwamko wa 15 Khordad ulikuwa mwamko wenye kufuata mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Ulikuwa mwamko wa Ikhlasi wenye lengo la kutekeleza wajibu wa kidini. Nukta ya tatu ya kipekee ya mwamko wa 15 Khordad ni kuwa ulikuwa mwamko wa wananchi na haukuwa mwamko wa tabaka maalumu. Watu wa matabaka yote katika miji, vijijini, vyuo vikuu, wanawake kwa wanaume, wazee kwa vijana wote walishiriki katika mwamko huu. Kile kilichowaleta pamoja watu hao wote ni Uislamu. Ulikuwa mwamko ambao haukufungamana na kambi ya Mashariki wala Magharibi. Ni nukta hizi ndizo zilizochangia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na ni nukta hizi hizi ambazo zimepelekea kupatikana ustawi na uwezo mkubwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hakuna shaka kuwa, kutokana na kuwa ya Kiislamu, yenye uungaji mkono wa wananchi na Kiongozi wa Mapinduzi anayepewa himaya na wananchi, Jamhuri ya Kiislamu imeweza kufanikiwa kukabiliana na uhasama wa Marekani na waitifaki wake katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita. Nukta hizi zimepelekea Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yawe mfano wa kuigwa na mataifa ya eneo yaliyoamka dhidi ya tawala vibaraka na tegemezi kwa Marekani. Kwa kuiga mfano wa Iran, wananchi wa eneo sasa wanapinga dhulma na wameshikamana na thamani za Kiislamu katika kupinga mielekeo yote ya kiliberali na isiyo ya kidini.
1021982
captcha