IQNA

Kanali ya televisheni ya al-Mayadin yaanzishwa mjini Beirut

17:05 - June 12, 2012
Habari ID: 2345407
Kanali ya televisheni ya al-Mayadin ilianzishwa jana Jumatatu mjini Beirut Lebanon kwa lengo la kutangaza habari na kuakisi matukio ya ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu na hasa kuhusu Palestina na Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Ghassani bin Jaddu ndiye anayeongoza bodi itakayosimamia uendeshaji wa televisheni hiyo itakayoendesha shughuli zake pembeni ya televisheni nyingine 700 zinazoakisi masuala ya ulimwengu wa Kiislamu.
Bin Jaddu ambaye alikuwa akifanya kazi na televisheni ya al-Jazeera ya Qatar amesema kuwa televisheni hiyo imeanzishwa baada ya juhudi kubwa za karibu miezi 9, jambo ambalo amesema limevunja rekodi katika uanzishaji wa televisheni za satalaiti. Amesema televisheni hiyo imeanzishwa katika mazingira nyeti ya hivi sasa katika nchi za Kiarabu na kwamba kuakisiwa matukio ya nchi hizo kwa njia sahihi ni jukumu muhimu la vyombo vya habari.
Amesema televisheni hiyo ambayo ina zaidi ya wafanyakazi 300 itakuwa ikitekeleza majukumu yake bila kuupendelea upande wowote na kwamba nara yake muhimu itakuwa ni kuunga mkono demokrasia na haki za binadamu.
Ameongeza kuwa moja ya majukumu muhimu ya televisheni hiyo itakuwa ni kuakisi matukio ya Palestina na Quds Tukufu. 1028202
captcha