'Ni kupitia tuu kuimarisha umoja na udugu pamoja na fikra ya Khilafa miongoni mwa Waislamu ndio Msikiti wa Al Aqsa unaweza kuokolewa kutoka makucha ya maadui wa Uislamu,' amesema Imam wa Masjid Al Aqsa, Profesa Sheikh Abu Mohammad Al Hamudi.
Ameyasema hayo katika sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Rahmatul Alam katika eneo la Banjjara jimboni Hyderabad nchini India.
Katika hotuba yake Profesa Al Hamudi alisisitia kuhusu udharura wa umoja miongoni mwa Waislamu na umuhimu wa kuundwa serikali moja ya mataifa yote ya Kiislamu duniani kwa msingi wa mfumo wa Khilafa.
'Kila Mwislamu duniani anatamani kuona Msikiti wa Al Aqsa ukiokombolewa kutoka udhibiti wa Wazayuni na Wakristo. Waislamu wanataka pia kuona nchi za Kiislamu zikikombolewa kutoka udhibiti wa madola ya kibeberu yanayoupinga Uislamu. Haya yote yanaweza kujiri tu kwa Umoja wa Waislamu chini ya utawala wa Ukhalifa wa Kiislamu,' amesema.
Katika hotuba yake amenukulu aya za Qur'ani na Hadithi za Mtume SAW kuhusu umuhimu wa umoja miongoni mwa Waislamu.
Imam Al Hamudi ambaye pia ni profesa wa sayansi za kibiolojia katika Chuo Kikuu cha Quds amesema Uislamu ndio njia pekee ya kuelekea peponi na kuongeza kuwa Uislamu ni njia ya maisha ambayo humfanya mwanaadamu awe kiumbe bora.
1036224