Kwa mujibu wa matokeo hayo Muhammad Mursi ameshinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 52 ya kura. Tume hiyo ya uchaguzi imemtangaza Mursi ambaye alikuwa mgombea wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin katika duru ya pili ya uchaguzi kuwa ndiye aliyeshinda uchaguzi huo na kumpita mpinzani wake Ahmad Shafiq katika uchaguzi huo muhimu katika historia ya Misri kwa kura karibu milioni moja. Mursi amepata kura milioni 13 na laki mbili na elfu 30 na kumpiku mpinzani wake Ahmad Shafiq ambaye alikuwa waziri mkuu wa mwisho wa utawala uliong'olewa madarakani wa Misri. Shafiq amepata kura milioni 12 lakini tatu na 47 elfu.
Tume ya Uchaguzi ya Misri imetangaza kuwa Wamisri milioni 25 walishiriki katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais idadi ambayo ni sawa na zaidi ya asilimia 50 ya jumla ya watu waliojiandikisha kwa ajili ya kupiga kura.
Rais mteule wa Misri Muhammad Mursi ni mwanasiasa aliyeongoza chama cha Uhuru na Uadilifu kinachofungamana na Harakati ya Ikhwanun Muslimina baad aya mapinduzi ya wananchi wa Misri mwaka 2011. Katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2005 Mursi alikuwa mbunge. Alipata elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Qairo na alihitimu shahada ya uzamivu kama mhandisi katika Chuo Kikuu cha California.
Uchaguzi wa rais wa Misri ulikuwa wa kwanza wa kidemokrasia katika historia ya nchi hiyo. Uchaguzi huo uliofanyika baada ya kipindi cha utawala wa kidikteta wa Hosni Mubarak ni hatua muhimu katika njia yenye mashaka mengi iliyoko mbele ya taifa la Misri. Hususan kwa kutilia maanani kwamba Baraza Kuu la Kijeshi lililoteuliwa na Hosni Mubarak limefanya jitihada kubwa za kutaka kuzuia ushindi wa Morsi katika uchaguzi huo. Wanajeshi wa Misri wametumia mbinu mbalimbali kwa ajili ya kudhibiti hali ya mambo kwa maslahi mabaki ya utawala uliong'olewa madaraka ikiwa ni pamoja na kulivunja bunge lililochaguliwa na wananchi, kubuni sheria zinazotumika kama sehemu ya katiba ya nchi, kudhibiti masuala ya usalama na bajeti ya taifa na wakati huo huo kubana mamlaka ya rais wa nchi.
Hapana shaka yoyote kwamba uchaguzi wa rais wa Misri ni mtihani mkubwa wa demokrasia kwa wananchi na watawala wa sasa wa nchi hiyo. Miaka 30 ya utawala wa kidikteta wa Hosni Mubarak katika nchi hiyo yenye utamaduni mongwe ilisababisha maafa makubwa na kuondolewa madarakani utawala huo ilikuwa hatua muhimu na ya dharura. Kwa msingi huo mapinduzi ya wananchi wa Misri ni fursa kwa Wamisri kwa ajili ya kujenga mustakbali mzuri zaidi.
Baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa Misri tunapaswa kusubiri na kuona jinsi muundo mpya wa kisiasa utakavyokuwa nchini humo. Vilevile hapana shaka kuwa rais mteule Muhammad Mursi anakabiliwa na kibarua na changamoto kubwa.
1037530