IQNA

Morsi asema Misri imezaliwa upya kupitia irada ya wananchi

12:03 - June 30, 2012
Habari ID: 2357230
Rais mteule wa Misri, Dk. Mohammad Morsi amesema kuwa, nchi hiyo imezaliwa upya kupitia nguvu na irada ya wananchi na kwamba hakuna mamlaka mengine yanayoshinda yale ya wananchi.
Morsi amesema hayo alipohutubia makumi ya maelfu ya Wamisri katika medani mashuhuri ya Tahrir mjini Cairo hapo jana Ijumaa.
Ameahidi kwamba ataendelea kuwa Rais wa wananchi wote bila ya kujali itikadi zao za kidini na kisiasa.
Katika kile kilichotajwa na weledi wa mambo kuwa ni kiapo cha urais, Dk. Morsi amesema, atatetea haki za Wamisri wote kwa ujasiri na jambo atakalolipa kipaumbele ni kupatikana katiba mpya itakayotokana na matakwa ya wananchi.
Amezungumzia kadhia ya Palestina na kusisitiza kuwa serikali yake itafanya juu chini kuwasaidia wananchi wa Palestina.
Amesisitiza kuwa Misri itadumisha uhusiano mzuri na mataifa ya dunia yanayozingatia misingi ya udugu na ushirikiano na wala hatokubali nchi yake kukoloniwa na wakoloni mamboleo.
Mohammad Morsi ataapishwa rasmi hii leo Jumamosi mbele ya jopo la majaji wa mahakama ya juu zaidi nchini Misri na atakuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia tangu nchi hiyo ipate uhuru.
1040838
captcha