Taarifa hiyo imesema kuwa turathi za Kiislamu zinazokusudiwa ni pamoja na misikiti, majengo ya kihistoria na nyaraka za kale zilizoandikwa kwa mkono. Imesema vyama na makundi yanayotawala mjini humo ndiyo yaliyo na jukumu la kulinda turathi hizo na kuwapa mafunzo wananchi kuhusiana na umuhimu na njia za kuzilinda.
Taarifa ya ISESCO imewataka Waislamu kufuata mfano na sera za Mtume Mtukufu (saw) katika kukabiliana na masuala mbalimbali. Imesisitiza kwamba wafuasi hao wanapasa kuwa na msimamo wa wastani katika kukabiliana na changamoto tofauti na kuepuka misimamo ya kupindukia mipaka kwa sababu Uislamu ni dini ya rehema na mienendo ya wastani.
Taarifa hiyo ya Isesco pia imezitaka nchi wananchama wa OIC kuchukua hatua za lazima katika kulinda turathi za kihistoria ambazo zinahusiana na ulimwengu wa Kiislamu na ustaarabu wa jamii nzima ya mwanadamu.
Siku ya Jumamosi Juni 30 makundi ya Kiwahabi yenye misimamo ya kupindukia mipaka na ambayo huwa hayaheshimu hata misingi ya wazi kabisa ya Uislamu yalichukua hatua ya kushangaza ya kubomoa makaburi ya kale ya mawalii wa Mwenyezi Mungu katika mji wa Timbuktu. Makaburi hayo yanayosimamiwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO yamebomolewa kufuatia ghasia za miezi mitatu kaskazini mwa Mali.
Timbuktu ni mji muhimu wa historia ya Kiislamu ambao mbali na turathi nyingine kongwe za Kiislamu una nyaraka za kale zipatazo 100,000 ambapo baadhi ni za karne ya 12. Nyaraka hizo kimsingi zinahifadhiwa kwenye nyumba au katika maktaba za watu binafsi ambao kimsingi ni wanazuoni wa kidini. 1043403