Taarifa ya OIC imetaka hatua zichukuliwe kulinda maeneo hayo ya kihistoria ya Mali na kusema turathi yenye historia ndefu na tajiri ya Kiislamu nchini Mali inapaswa kuhifadhiwa.
Waasi kutoka kundi linalojiita Ansar Din nchini Mali walivunja makaburi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu katika mji mkongwe wa Timbuktu kaskazini mwa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika.
Duru za habari zinasema makaburi hayo ya Mawalii wanaoheshimiwa na Waislamu wa mji huo wenye itikadi ya Kisufi yalivunjwa na waasi hao siku ya Jumamosi Juni 30.
Tayari waasi wenye kufurutu mipaka wa Ansar Din walikuwa wameshabomoa makaburi ya mawalii wakiwemo Sidi Mahmoud, Sidi El Mokhtar, na Alfa Moya.
Kundi lenye misimamo mikali la Ansar Din pamoja na waasi wa Tuareg walichukua udhibiti wa eneo la kaskazini mwa Mali ikiwa ni pamoja na mji wa kale wa Timbuktu baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Machi 22 nchini humo.
Kundi la Ansar Din linalofuata itikadi za kufurutu ada za Kiwahabi linapinga mila na desturi za Kiislamu za kufanya ziara katika makaburi ya Mawalii. Kundi hilo limeapa kuteketeza moto makaburi na nyaraka za kale za Kiislamu mjini Timbuktu.
Juzi Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO liliuweka mji wa Timbuktu katika orodha ya miji ya kale inayokabiliwa na tishio la kuangamia.
1043427