Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, mji wa Mumbai sasa umegawanyika katika misingi ya kidini, lugha na vyakula.
Mtangazaji wa Radio Yunus Khan anasema: ‘Nilikuwa natafuta nyumba na maajenti walinifahamisha kuwa haiwezekani kupata nyumba katika eneo la Gorai. Wanasema Waislamu hawatakikani katika eneo hilo.”
Kaka yake Khan pia alipata tatizo kama hilo wakati alipojaribu kukodisha nyumba katika mtaa wa Charkop katika eneo la Kandivali.
Tokea mashambulio ya mwaka 2008 yaliyopelekea kuuawa watu 172, wengi wao wakiwa Waislamu, hivi sasa Waislamu wa Mumbai, ambao ni karibu watu milioni 2 kati ya milioni 19, wanaishi kwa hofu kubwa ya kulengwa kutokana na itikadi yao.
Waislamu wa Mumbai wana haki ya kuwa na wasiwasi. Katika machafuko ya mwaka 1992-1993 mjini Mumbai, Waislamu zaidi ya 1000 waliuawa. Machafuko hayo yalifuatia hatua ya Mabaniani au Wahindu wenye misimamo mikali kubomoa Msikiti wa karne kadhaa katika mji wa Ayodhya wa kaskazini mwa India.
Waislamu wa mji mkuu wa kisiasa wa India New Delhi pia wanakabiliwa na ubaguzi.
Kwa muda mrefu Waislamu nchini India wamekuwa wakilalamika kuwa wanabaguliwa katika nchi hiyo inayotawaliwa na Mabaniani. Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa Waislamu ni takribani asilimia 13 ya watu bilioni 1.1 nchini India.
1048689