Katika taarifa iliyotolewa kufuatia kuuawa shahidi vijana wawili wa Kishia na kutiwa nguvuni Sheikh Nimr an Nimr mmoja kati ya wanazuoni wa Kishia Saudia, Maulamaa wa Kishia wameashiria sera za kubaguliwa Mashia za Aal Saud. Aidha wametaka wafungwa wote wa kisiasa wa Kishia waachiliwe huru.
Kama tunavyoshuhudia, Saudi Arabia hivi sasa inapitia katika siku zilizojaa misukosuko. Matukio ya hivi karibuni mashariki mwa Saudia na kuongezeka maandamano ya wananchi katika eneo hilo ni kengele ya hatari kwa utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Saud.
Waandamanaji wamekuwa wakitoa nara za kutaka mabadiliko katika mfumo wa kisiasa unaotawala Saudi Arabia. Aidha wametoa nara za kutaka kuangusha utawala wa Aal Saud. Katika siku za hivi karibuni miji ya Qatif na Awamiyyah huko mashariki mwa Saudia imegeuka na kuwa medani ya maandamano makubwa ya wananchi wanaotaka utawala wa Aal Saud upinduliwe. Maandamano hayo yamehujumiwa na vikosi katili vya kijeshi ambapo watu kadhaa wameuawa shahidi na wengine kujeruhiwa vibaya. Kati ya waliojeruhiwa ni Sheikh Nimr an Nimr mwanazuoni maarufu wa Kishia Saudia ambaye tayari ameshatiwa mbaroni na vikosi vya usalama. Kutiwa nguvuni mwanzuoni huyo kumepelekea kuongezeka machafuko mashariki mwa Saudia na wananchi wameazimia kukabiliana na watawala madhalimu.
Imebainikwa kuwa watawala wa Saudia wameingiwa na wasi wasi mkubwa sana kutokana na machafuko hayo. Kile wanachoogopa ni kuenea mwamko wa mashariki hadi maeneo yote ya Saudi Arabia. Kwa kuzingatia hilo eneo la mashariki mwa Saudia sasa limeanza kutawaliwa kijeshi ili kudhibiti hali ya mambo. Imedokezwa kuwa watawala wa ukoo wa Aal Saud wameazimia kutoka wanajeshi zaidi ya elfu tatu katika eneo la mashariki linalokumbwa na machafuko. Aidha wanajeshi wote Saudi waliokuwa likizoni wametakiwa kurejea kazini mara moja na sasa wako katika hali ya tahadhari huku wakijitayarisha kuelekea katika miji ya Qatif na Awamiyyah. Kati ya vikosi vitakavyotumwa mashariki mwa Saudia ni vile vila 'Gadi ya Kitaifa' ambavyo vinasimamiwa na mwanamfalme Mutaib bin Abdulaziz Aal Saud. Lengo la kutumwa vikosi hivyo katika eneo la mashariki ni kujaribu kukandamiza mwamko wa wananchi. Lakini suali linalojitokeza hapa ni hili, je, sera za kutumia mabavu na silaha zinaweza kuzima kilio cha watu wanaopigania haki na uhuru? Saudi Arabia inaendeshwa kwa mfumo wa kale wa kisiasa uliojengeka kwa msingi wa utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Saud unaosimamia kila kitu nchini humo. Mfumo huo wa kiimla umejengeka katika misingi ya taasubi za kimadhehebu za kundi la waliowachache. Suala hili limekuwa likipingwa kwa miaka mingi lakini sauti za wanyonge wanaopigania uadilifu zimekuwa zikizimwa kwa mkono wa chuma wa ukoo wa Aal Saud. Lakini hivi sasa hali ya ndani ya Saudia imeathiriwa na Mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa katika katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika. Kwa kuzingatia hilo, ukoo wa Aal Saud umeingiwa na kiwewe na umeamua kutumia nguvu za kijeshi kukandamiza mwamko wa wananchi. Lakini uzoefu unaonyesha kuwa kutumia nguvu za kijeshi hakutakuwa na natija nyingine ila kuimarisha irada ya wananchi kupigania haki zao. Ni wazi kuwa misingi ya ukoo wa Aal Saud imetikisika na hatima yake itakuwa sawa na ya madikteta wengine katika eneo ambao wanaanguka moja baada ya mwingine.
1051692