IQNA

Mpango wa Annan Syria, makabiliano baina ya mirengo ya amani na vita

23:41 - July 16, 2012
Habari ID: 2369847
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika mgogoro wa Syria amesema kwamba, Wamagharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu ambazo ni waitifaki wao ndio chanzo kikuu cha kuendelea machafuko nchini Syria. .
Aidha amesisitiza ulazima wa Iran kushirikishwa katika utatuzi wa mgogoro wa Syria.
Kofi Annan amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Kifaransa la Le Monde. Alisisitiza kinagaubaga kwamba maadamu Wamagharibi na baadhi ya tawala za Kiarabu katika Mashariki ya Kati hazijakomesha hatua zao za kuvuruga mambo nchini Syria, nchi hiyo itaendelea kukabiliwa na tishio la kutumbukia katika vita vya ndani. Annan amesema, licha ya juhudi alizofanya kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria lakini amefikia natija hii kwamba, jithada zake hizo zimeshindwa.
Bwana Annan aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, moja ya sababu za kimsingi zilizokwamisha mpango wake ni uingiliaji wa wazi wa baadhi ya madola makubwa katika masuala ya ndani ya Syria. Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika mgogoro wa Syria ameashiria pia nafasi ya Russia katika kukwamisha aina yoyote ile ya hatua ya kimataifa dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad na kusisitiza kwamba, ni lazima Iran iwepo katika mazungumzo yanayohusiana na Syria.
Matamshi ya Kofi Annan yanatolewa siku moja tu baada ya kufanyika kikao cha wale wanaojulikama kama "Marafiki wa Syria" ambacho kimetaka kuwekewa vikwazo zaidi serikali ya Damascus; kikao ambacho kilisusiwa na Annan mweyewe.
Mpango wa Kofi Annan kwa ajili ya Syria uliotolewa Februari mwaka huu, unatathminiwa na wachambuzi wa mambo kuwa ilikuwa jitahada muhimu kabisa za jamii ya kimataifa za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo. Mpango huo ulikuwa na vipengee sita ambavyo ni kusitishwa operesheni za kijeshi dhidi ya raia, vikosi vya kijeshi kuondoka katika maeneo ya mijini, kutolewe ruhusa ya kufanyika maandamano ya amani, wafungwa wa kisiasa waachiwe huru, pande zinazopigana kila siku zisitishe mapigano kwa muda wa masaa mawili ili kuruhusa kupelekwa misaada katika maeneo ya vita na vile vile pande mbili zianze mazungumzo ya kisiasa yenye lengo la kuutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Rais wa Syria sambamba na kukaribisha mpango huo wa Annan alitangaza kufungamana nao; lakini waasi wanaobeba silaha mbali na kupuuza mpango huo wameendelea kufanya mauaji dhidi ya raia huku wakiharibu maeneo ya umma na ya serikali. Wataalamu wa mambo wanaamini kwamba, siasa za kindumakuwili za Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu kama alivyosema Kofi Annan ndizo zinazokwamisha utatuzi wa mgogoro wa Syria. China na Russia ni wapinzani wakuu wa siasa za Marekani na Ulaya kuhusiana na matukio ya Syria na zimeonya mara kadhaa kuhusiana na hatua yoyote ile ya kuingia kijeshi katika ardhi ya Syria.
1053306
captcha