Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Ramin Mehmanparast amesema: 'Inatarajiwa kuwa serikali ya Myanmar itachukua hatua za kuimarisha mshikamano, umoja wa kitaifa na kulinda haki za Waislamu nchini humo ili kuzuia maafa zaidi.'
Aidha ametaka hatua za haraka zichukuliwe na serikali ya Myanmar, jamii ya kimataifa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kwa lengo la kuchunguza na kubainisha chanzo cha mauaji ya Waislamu katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia.
Tokea mwezi Juni mwaka huu wa 2012, mamia ya Waislamu wa kabila la Rohingya wameuawa na makumi ya maelfu ya wengine kuachwa bila makao kufuatia machafuko yaliyozuka mashariki mwa Myanmar. Idadi ya Waislamu wa kabila la Rohingya ni karibu milioni moja kati ya watu milioni 47 nchini Myanmar.
Juni 3 Waislamu 10 wa kabila la Rohingya waliuawa na genge la Mabuddha lijulikanalo kama Rakhines.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema tangu Juni 10-28 Waislamu 650 wa kabila la Rohingya waliuawa, 1,200 wametoweka na hawajulikani waliko na wengine 80,000wameachwa bila makao. Jeshi la Myanmar linalaumiwa kwa kuongoza kampeni ya kuwakandamiza Waislamu.
Myanmar ambayo zamani ikijulikana kama Burma ni nchi iliyo kusini mashariki mwa Asia na inapakana na India, Bangladesh, China, Laos na Thailand.
1055058