Akizungumza na IQNA, Ali Ridha Buzhmehrani, mwanachama wa Jopo la Kuainisha Mwezi Mwandamo katika Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amefafanua kuhusu harakati za kuainisha mwezi mwandamo katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na kusema: 'Tarehe 29 Shaaban (Alkhamisi Julai 19) si tu kuwa hilali ya Ramadhani haitaweza kuonekana Iran, bali pia haitaweza kuonekana katika nchi yoyote ya Kiislamu kwa macho wala chombo (teleskopu).'
Amefafanua kwa kusema: 'Tarehe 29 Shaaban (19 Julai) mwezi utazama (ghurub) mapema zaidi ya jua na kwa hivyo wakati jua linapozama mwezi hautaweza tena kuonekana angani na hakuna haja ya kuenda kuutafuta mwezi mwandamo,'.
Ali Ridha Buzhmehrani ameongeza kuwa: 'Katika nchi za Kiislamu zinazopakana na Iran zikiwemo zilizo katika Ghuba ya Uajemi, hali itakuwa ni hii hii na pengine katika baadhi ya nchi hizo mwezi utazama kwa wakati mmoja na jua lakini parameta za hilali au mwezi mwandamo zitakuwa dhaifu kiasi kwamba hakutakuwepo uwezekano wa kuuona hata kwa teleskopu.'
Mtaalamu huyo amesema hali itakuwa hivyo katika nchi za Kiislamu barani Afrika na halikadhalika katika nchi za Kiislamu za Mashariki na Kusini mwa Asia. Kwa kuzingatia hilo Siku ya Alkhamisi 29 Shaaban/19 Julai mwezi mwandamo hautaweza kuonekana katika nchi yoyote ya Kiislamu.
1054628