Shughuli za siku ya leo zimeitishwa na baadhi ya asasi siziso za serikali na kuwataka Waislamu katika nchi mbalimbali kuandamana kwa lengo la kuonyesha mshikamano wao na Waislamu wenzao wanaouawa kwa umati huko Myanmar. Mjini London huko Uingereza shughuli za siku ya kimataifa ya kuonyesha mshikamano na Waislamu wa Myanmar zimefanyika mbele ya ubalozi wa nchi hiyo kuanzia saa 12.5 hadi 1.5 jioni kwa wakati wa London huku wakazi wa Bombei na new Delhi huko India wakikusanyika mbele ya ofisi za Umoja wa Mataifa kupinga mauaji ya Waislamu huko Myanmar.
Waislamu katika nchi za Malaysia, Indonesia na Uturuki, Misri, Japan, Ghaza na kwengineko pia wamekusanyika leo katika siku ya kimataifa ya kuonyesha mshikamano wao na Waislamu wa Myanmar.
Waislamu wa jiji la Tehran hapa nchini Iran pia wamekusanyika mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa wakitangaza upinzano wao dhidi ya mauaji ya Waislamu wenzao nchini Myanmar. Tokea mwezi Juni mwaka huu wa 2012, maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya wameuawa na makumi ya maelfu ya wengine kuachwa bila makao nchini Myanmar.
Umoja wa Mataifa umesema kuwa madhila wanayopitia Waislamu wa Myanmar ndiyo makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika siku za hivi karibuni duniani. Serikali ya Myanmar imekataa kutambua jamii ya Waislamu nchini humo ikidai kwamba wao si raia halali na kwamba wanatambuliwa tu kama wahajiri haramu.1061219