IQNA

Serikali ya Kenya kufadhili madrasa za Qur'ani

14:18 - July 25, 2012
Habari ID: 2377214
Serikali ya Kenya imeidhinisha sheria mpya inayosema kuwa shule za Kiislamu zitaingizwa katika mfumo rasmi wa masomo nchini Kenya.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation toleo la tarehe 24 Julai, aidha mfumo wa shule za Kiislamu ujulikanao kama Duksi utaingizwa katika masomo rasmi ya shule katika maeneo yenye Waislamu wengi nchini humo. Mfumo wa Duksi aghalabu hutumiwa na jamii ya Wakenya wenye asili ya Somalia na unajumuisha kuhifadhi Qur'ani na masomo mengine ya Kiislamu.
Katibu wa Kudumu katika Wizara ya Elimu Profesa Geroge Godia shule hizo za Kiislamu ziitapata msaada rasmi wa kifedha kutoka kwa mfuko wa serikali. Ameongeza kuwa kwa mujibu wa muswada wa sheria kuhusu Elimu ya Msingi Mwaka 2012, ni jukumu la serikali kuwalipia karo wanafunzi wa madrasa za Kiislamu na pia kuwapa chakula wakiwa katika madrasa.
Waziri wa Elimu wa Kenya Mutula Kilonzo amesema uamuzi huo wa serikali unaenda sambamba na katiba mpya pamoja na mpango wa miaka 20 wa maendeleo Kenya.
Wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na Sheikh Mohammad Khalifa Wa Baraza la Maimamu na Wahubiri ameipongeza hatua hiyo ya serikali. Ametoa wito kwa serikali kuidhinisha rasmi sheria ya kuwapa haki wasichana wa Kiislamu kuvaa hijabu.
1061402

captcha