IQNA

CAIR yatoa wito wa kulindwa jamii ya Waislamu Myanmar

17:04 - August 04, 2012
Habari ID: 2385243
Baraza la Uhusiano wa Kiislamu na Marekani (CAIR) limezitaka serikali za Myanmar na Bangladesh kuwalinda Waislamu wa Myanmar ambao wanakabiliwa na wimbi jipya la ukatili na manyanyaso.
Jumuiya ya CAIR pia imeitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kupunguza mashaka yanayowapata karibu Waislamu milioni moja wa Myanmar na wale waliokimbilia nchini Bangladesh.
Hivi karibuni shirika la kutetea haki za binadamu na Human Rights Watch liliripoti kuwa jeshi la Myanmar limekuwa likitenda ukatili na kuwaua Waislamu nchini humo tangu miezi kumi iliyopita na kwamba maelfu ya Waislamu hao wameuawa na wengine wengi kukimbia nyumba zao. Shiriki hilo limesema Waislamu wa Myanmar wanahitaji chakula makazi na misaada ya tiba.
Wakati huo huo wananchi wa Misri wamefanya maandamano mbele ya ubalozi wa Myanmar nchini humo na kuiteremsha bendera ya Myanmar.
Habari zinasema kuwa, wananchi hao waliokuwa wamejawa na hasira wamelaani vikali mauaji ya Waislamu wa Myanmar sambamba na kuushambulia ubalozi na kuiteremsha bendera ya nchi hiyo kutoka katika paa la ubalozi huo na kuichoma moto. Aidha waandamanaji hao waliokuwa wakitoa nara za kutaka kumfukuza balozi wa Myanmar nchini Misri, wametaka pia serikali ya Cairo kukata uhusiano na nchi hiyo isiyojali sheria za kimataifa.
Mjumbe wa harakati ya Kiislamu iitwayo Jamaatul Islami, Asim Abdul Majid amesema, wajumbe wa makundi tofauti ya wanamapinduzi walishiriki maandamano hayo ya kulaani mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu wa Myanmar na kuitaka serikali ya Misri kumfukuza balozi huyo nchini kwao.
Naye sheikh Madh'har Shahin mmoja wa makhatibu wa swala za Ijimaa nchini Misri amezilaumu nchi za Kiarabu na za Kiislamu kwa kuzembea dhidi ya mauaji ya Waislamu nchini Myanmar na kusema kuwa, nchi hizo zinapaswa kuchukua hatua kali dhidi ya Myanmar sambamba na kuwafukuza mabalozi wa nchi hiyo katika nchi za Kiarabu na Kiislamu. 1070480

captcha