IQNA

Waislamu wa Ufaransa waandamana kupinga chuki dhidi yao

17:08 - August 05, 2012
Habari ID: 2386100
Waislamu wa mji wa Gennevilliers nchini Ufaransa wamefanya maandamano makubwa mbele ya majengo ya meya katika mji huo kwa lengo la kulaani hatua ya kuachishwa kazi wafanyakazi wanne wa Kiislamu kwa kufunga saumu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na pia kupinga kuenea chuki dhidi yao na dhidi ya Uislamu nchini humo.
Maafisa wa ofisi ya meya mjini humo wamedai kwamba wafanyakazi hao walifutwa kazi kwa kuwa hawangeweza kutekeleza vyema majukumu yao ya kuwahudumia watoto waliokuwa wakiwasimamia katika kambi ya mapumziko ya msimu wa joto wakiwa wamefunga.
Washiriki wa maandamano hayo wamesema wameandaa maandamano hayo kwa lengo la kutangaza mfungamano wao na wafanyakazi hao wa Kiislamu waliofutwa kazi kwa kutii amri ya dini yao. Wamesema lengo lao jingine ni kuwatangazia watawala wa Ufaransa kwamba saumu haikinzani kwa vyovyote vile na shughuli za kila siku.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa na kijamii vya nchi hiyo wamesema kwamba hatua ya meya ya kuwaachisha kazi wafanyakazi hao wa Kiislamu ilitokana na sababu za kisiasa.
Waislamu wa Ufaransa wamekuwa wakilalamikia vikali chuki na ubaguzi unaofanywa dhidi yao katika idara, shule, vyuo vikuu, mikahawa, kazini na maeneo ya umma nchini humo.
Kuzuiwa kuswali katika maeneo ya umma na pia kuvalia vazi la hijabu ni baadhi ya hatua ambazo zimechukuliwa na serikali ya Paris dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. 1071261
captcha