IQNA

OIC yataka kulindwa haki za Waislamu duniani

18:02 - August 05, 2012
Habari ID: 2386181
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa taarifa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu za Kiislamu ikitaka kulindwa haki za Waislamu katika maeneo ambayo wafuasi wa dini hiyo ni wachache kote duniani.
Katibu Mkuu wa OIC Ekmeleddin Ihsanoglu amesema katika taarifa hiyo kwamba mwaka huu Siku ya Kimataifa ya Haki za Kiislamu duniani inaadhimishwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na hii ni fursa nzuri kwa nchi wanachama wa OIC kuchukua azma zaidi ya kutekeleza haki za binadamu katika ulimwengu wa Kiislamu.
Amesema kuwa jumuiya ya OIC imeazimia kuimarisha haki za binadamu na uhuru katika nchi wanachama kwa mujibu wa mpango wa miaka 10 uliopasishwa katika mkutano wa mwaka 2005 mjini Makka.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya ushirikiano wa Kiislamu ameshiria pia hali ya wananchi wa Palestina na kusema maghasibu wa Kizayuni wangali anashikilia ardhi za Palestina kwa miaka mingi sasa na kwamba mashaka na machungu yanayowapata wananchi wa Palestina ni mfano wa wazi wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
Ameelezea kusikitishwa na ukiukwaji wa haki za Waislamu katika nchi zisizo za Kiislamu hususan huko Myanmar ambako haki za binadamu za Waislamu hao zinakanyagwa kwa kuuawa kinyama, kubakwa na kufukuzwa katika makazi yao.
Katibu Mkuu wa OIC amezitaja nchi za Kiislamu kuishinikiza jamii ya kimataifa ili ichukue hatua haraka za kutetea haki za binadamu za Wapalestina na Waislamu wa Myanmar. 1071535

captcha